Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi amtembelea Mzee Hassan Omar Mzee Kituo cha Afya Kibweni

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsalimia na kumjulia hali Mzee Hassan Omar Mzee alipofika Kituo cha Afya Kibweni Wilaya ya Magharibi"A" Mkoa wa Mjini Magharibi.[Picha na Ikulu] 24/12/2021.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Magendo KMKM Komodoo Azana Hassan Msingiri (katikati) mara baada ya kumjulia hali Mzee Hassan Omar Mzee aliyelazwa katika Kituo cha Afya Kibweni Wilaya ya Magharibi"A" Mkoa wa Mjini Magharibi (kushoto) L.Kamanda Mwashamba Mbarouk Salum .[Picha na Ikulu] 24/12/2021. 
 

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

 Zanzibar                                                                                     24.12.2021

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ya kuzimarisha huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuziimarisha Hospitali za Vikosi hapa Zanzibar.

 

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika Hospitali ya Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Kibweni mara baada ya kumkagua Bwana Hassan Omar Mzee ambaye ni mgonjwa pamoja na kuangalia mazingira ya Hospitali hiyo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa azma hiyo haitokuwa kwa hospitali pekee za Serikali bali itahusisha mpaka hospitali za Vikosi sambamba na kuwa na mpango mzuri wa kutoa dawa kutoka katika Bohari ya Serikali na kuzisaidia Hospitali hizo ikiwemo Hospitali hiyo ya (KMKM) iliyopo Kibweni, Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Hospitali hiyo pamoja na zile nyengine za vikosi zimekuwa zikitoa msaada mkubwa wa huduma za afya kwa wananchi jambo ambalo Serikali imeona haja ya kukiongezea nguvu na kukiunga mkono ili kizidi kutoa huduma hizo kwa ufanisi mkubwa.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Hospitali hiyo ya (KMKM) iliyopo Kibweni kwa juhudi zake kubwa inazozichukua katika kutoa huduma za afya kwa wananchi na kutaka juhudi ziongezwe ili hospitali hiyo iwe bora zaidi.

Aidha, alisisitiza kwamba Serikali kwa upande wake itasaida kutatua changamoto zinazoikabili hospitali hiyo ili iwe moja wapo ya Hospitali inayotoa huduma bora za afya kwa wananchi ili hospitali hiyo iwe moja wapo inayotegemewa katika mji wa Zanzibar.

Alisema kuwa Serikali ina mpango wa kuifanyia matengenezo makubwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na kujenga Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi katika eneo la Lumumba ambapo uwepo wa Hospitali hiyo ya (KMKM) Kibweni pia, itasaidia na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Nae Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Komodoo Azanna Hassan  Msingiri alieleza kwamba kwa siku Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wapatao 300, ambapo wananchi wamekuwa wakivutika sana na huduma zinazotolewa Hospitali hapo hasa kliniki za moyo, presha, kisukari na nyenginezo.

Aliongeza kwamba hospitali hiyo hivi sasa iko katika Hospitali ya Wilaya na bado ina mpango wa kupanda zaidi na kuwa ya Mkoa kutokana na mikakati ya ujenzi na huduma zinazotolewa Hospitalini hapo sambamba na kuongeza wataalamu mbali mbali.

Akiwa Hospitalini hapo, Rais Dk. Mwinyi pia, alipata nafasi ya kumkagua na kumjuulia hali Bwana Omar Hassan Mzee ambaye ni mmoja wa kati ya watu watatu waliobeba udongo wa Zanzibar na kuuchanganya na ule wa Tanganyika  mnamo Aprili 26, 1964 aliyelazwa Hospitali hapo akipatiwa matibabu.

Mapema, Alhaj Rais Dk. Mwinyi aliuangana na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa huko Masjid Jamiu Zinjibar Mazizini, Jijini Zanzibar ambapo baada ya sala hiyo waumini walitumia fursa hiyo kumshukuru na kumuombea dua ikiwa ni pamoja na dua na shukrani kwa kuwarejeshea wananchi fedha zao zilizochukuliwa na Kampuni ya Mastarlife.

Akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Rashid Salim Daudi alisisitiza suala zima la maadili katika jamii ikiwa ni pamoja na kukataza hujuma ndani ya ndoa kati ya mume na mke pamoja na kueleza haja ya kufuata mambo mema na kuachana na mambo maovu.

Imetolewa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.