Habari za Punde

Mrisho Kikwete ni Babu Yangu –Mhe Jakaya Kikwete.


Na.Adeladius Makwega. -Dodoma.

Jumapili ya Januari 30, 2022, kwa wale wasomaji wa matini zangu watakumbuka kuwa niliandika juu matini iliyopewa jina Maamuzi ya Hakimu Mrisho Kikwete.

Katika shauri hilo hakimu Mrisho Kikwete ambaye alikuwa akihudumu katika Mahakama ya Mwanzo ya Msoga mwaka 1944 alipokea shauri mezani kwake la kosa la jinai baina ya Mbone Lunema dhidi ya Makinamsisi.

Shauri hilo lilikuwa la ndugu hawa waliokuwa katika ngoma na Makinamsisi alipopomsukuma na kusababisha Mbone Lunema kuanguka na kupoteza meno yake mawili. Ndugu Mbone Lunema akaenda mahakamani kushitaki. Ndugu hawa wote walikuwa Wakwere wa koo zenye utani.

Mbele ya mahakama iliyo chini ya Hakimu Mrisho Kikwete shauri hilo lilitupiliwa mbali kwa kuwa lilikuwa shauri la kimila ulikuwa ni utani, shida ni Mbeno Lunemo mwenyewe ambaye aling’oka meno yake mawili kutokuwa makini na utani huo uliofanywa na Makina msisi.

Katika matini yangu nilieleza kuwa maelezo haya yalinukuliwa na Profesa Tigiti Sengo ambaye mwaka 1972 alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu ambaye alienda Kijijni Msoga kufanya utafiti juu ya utani baina ya kabila la Wakwere na namna mashauri hayo yalivyoamuliwa mbele ya mahakama.

Profesa Sengo alielezwa haya juu shauri hilo na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Msoga, Bagamoyo (Sasa Chalinze) Juni 1972 Mheshimiwa Bakari Mgweno ambaye shauri hilo wakati likiamuliwa mwaka 1944 alishuhudia kwa macho yake.

Kwa mujibu wa maandishi ya Profesa Sengo mwaka huo 1972 alipatiwa pia nakala ya mwenendo wa shauri hilo hadi lilipotupiliwa mbali.

Katika matini yangu niliuliza swali. Je Hakimu Mrisho Kikwete ni baba wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete?

Swali hili lilikuwa na sentensi yangu ya mwisho katika matini hiyo.

Binafsi niliwatafuta rafiki zangu na ndugu zangu Wakwere wanaoishi Msoga na Lugoba ilikuweza kulijibu swali hilo. Nilipowasiliana nao kwa njia ya simu waliniunganisha na Mwalimu Michael Mbena Kigunia ambae ni mwalimu mstaafu mwenye umri wa miaka 82.

Mwalimu huyu alieleza kuwa yeye anaifahamu vizuri familia ya Kikwete tangu enzi kuanzia Babu, Baba na ndugu zake wengine ambao kwa sehemu kubwa alisema waliishi nao tangu mazingira ya nyumbani hadi shuleni.

“Familia ya Kikwete walikuwa na maisha ambayo wakizalisha chakula cha kutosha kwa kwao, hawakuangaika na njaa na hata shuleni wengi wao walisoma tangu wakati huo.”

Mwalimu Mbena alienda mbali zaidi na kulijibu swali langu kwa kuniambia hakimu Mrisho Kikwete alikuwa Babu wa Jakaya Kikwete.

Mwalimu huyu alisema kuwa anamfahamu vizuri Hakimu Kikwete kwani wakati huo mahakama ya Msoga ilikuwa ni mahakama kubwa na maarufu huku ikihudumia Wakwere Wengi.

Kwa bahati nzuri, Februari mosi, 2022 saa 8.41 mchana nilipata jibu la swali hilo kutoka kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mwenyewe, Aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwanakwetu kabla sijalisema jibu hilo alilonipa niliwakumbuka walimu walionifundisha Shahada yangu ya Sanaa ya Habari kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa kama Dkt Irene Mkini, Dkt Gasper Mpehongwa na Profesa Esau Ntabindi walinifundisha kuwa mara nyingi maneno yanayosemwa na Kiongozi Mkubwa kama unayaandika kumbuka kuyanukuu kama yalivyo na yawekewe alama za kufunga na kufungua semi.

“Mrisho Kikwete alikuwa babu yangu aliyemzaa baba yangu Kikwete Mrisho Kikwete kwa jina lingine Halfani Mrisho Kikwete. Yeye alikuwa Mtawala na moja ya majukumu yake ni kusikiliza na kuamua mashauri ya kimila ya kabila la Wakwere yanayoletwa kwake.”

Alinijibu swali langu mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Binafsi namshukuru sana mheshimiwa Jakaya kikwete, kwanza kwa kuisoma matini yangu hiyo ya Maamuzi ya Hakimu Mrisho Kikwete na kwa namna ya pekee na kwa heshima na taadhima, namshukuru pia kwa kutoa jibu juu ya swali hilo nililofungia matini yangu.

Kitendo cha Mheshimiwa Jakaya Kikwete mwenyewe kujibu swali hili ni cha kiungwana na kinapaswa kuigwa na viongozi wengine kwani kama kuna jambo linakuhusu uugwana ni kulitolea ufafanuzi, kwani kiongozi ni mtu wa watu.

“Nakutakia kazi njema, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Mwenyezi Mungu akujali afya njema wewe na familia yako-Ahlan wa Sahlan.”

Kwa msomaji wa matini zangu, nakutakia siku njema na matini ijayo italihusu kabila la Wakerewe.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.