Habari za Punde

Uzinduzi wa Kituo cha Afya Kidimni Wilaya ya Kati Unguja leo.

 

                                                                                                                                                                                                     Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kuhakikisha kituo cha  Afya Kidimni kinakuwa na wataalamu wa huduma zote zinazopatikana kituoni hapo pamoja na watumishi  wengine wa Kada za Afya.

Dk. Mwinyi ametoa  wito huo katika hafla ya ufunguzi  wa Kituo cha Afya Kidimni, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho, kunaifanya Serikali kubeba dhima ya kuhakikisha kunakuwepo wataalamu na watumishi wanaohitajika, pamoja na kukipatia kituo hicho Dawa za kutosha.

Alisema kufunguliwa kituo hicho kunaleta faraja kubwa kwa wananchi, kwani kutawasogezea karibu huduma za Afya ambapo kabla walilazimika kuzifata  maeneo ya mbali.

Alisema baadhi ya huduma zitakazotolewa katika kituo hicho hazipatikani kwenye vituo vya Afya ya karibu, hususan huduma za uchunguzi wa maradhi, hivyo akatanabahisha kuwa kituo hicho kitapokea wananchi wengi kutoka maeneo tofauti.

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha huduma za Afya nchini zinatolewa kwa ufanisi mkubwa na kusisitiza azma ya Serikali ya kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuimarisha miundombinu, upatikanaji wa wataalamu, dawa pamoja vifaa tiba.

Alisema ili kufikia dhamira hiyo, Serikali inaendelea na hatua za ujenzi wa Hospitali kumi za Wilaya Unguja na Pemba, ambapo kwa Wilaya ya Kati Hospitali hiyo itajengwa eneo la Mwera Pongwe, huku Wilaya Kusini ikijengwa eneo la Kitogani.

“Mbali na Hospitali hizo tunaendelea na dhamira ya kujenga Hospitali ya Rufaa ambayo pia itakuwa Chuo cha kufundishia Madaktari pale Binguni, Mkoa Kusini Unguja”, alisema.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa washirika wa Maendeleo, zikiwemo taasisi  zisizo za Kiseriakli pamoja na taasisi za madhehebu ya  Dini kwa kuiunga mkono Serikali katika kurahisisha na kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya nchini.

“Natoa shukurani kwa  marafiki zetu wa taasisi ya Good People ya Korea Kusini na Taasisi isiyo ya Kiseriakli ya NOAH Development Association pamoja na Wananachi wakiwemo wa Kidimni kwa kushirkiana pamoja na kufanikisha ujenzi wa kituo hiki”, alisema.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi amezitaka Wizara za Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara Afya , Ustawi wa Jami, Wazee, Jinsia na Watoto, kuanza kujipanga na kutoa matangazo ya nafasi za Ajira, huku akisisitiza mkazo zaidi uwekwe kwa wafanyakazi waliokuwa wakijitolea.

Alisema Serikali inajipanga kutoa ajira katika Kada ya Afya ili kuwa na wafanyakazi wa kutosha katika majengo yaliojengwa pamoja na yale yanayoendelea kujengwa.

Nae, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui alisema mafanikio ya ujenzi wa kituo hicho cha Afya yanatokana na hatua ya Jumuiya hizo kujisajili hapa nchini baada ya kukidhi viwango, huku akibainisha kuwa urasimu ni kikwazo katika maendeleo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Hadid Rashid Hadid  aliishukuru Jumuiya ya  NOAH na kusema pamoja na kujikita katika kusaidia shughuli za kijamii katika Mkoa huo, pia imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia ujenzi wa skuli ya Maandalizi Kidimni, kusaidia vitendea kazi katika Ofisi za Serikali (Wilaya na  Mkoa) pamoja na kutoa huduma kwa jamii ya watu wenye Ulemavu.

Mapema, Balozi wa Korea Kusini  nchini Tanzania Kim Sun Pyo, alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maslahi ya Mataifa hayo na wananchi wake.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Fatma Mrisho alizishukuru Jumuiya za Good People na NOAH kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha Afya, ambapo hadi kukamilika kwake  kimegharimu zaidi ya shilingi Milioni 355.6/-, ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechangia eneo la Ardhi, huduma za umeme, wafanyakazi pamoja na msamaha wa kodi kwa vifaa vya ujenzi .

Alisema kituo hicho kitakachotoa huduma mbali mbali, kina uwezo  wa kuwahudumia wananchi wapatao 14,408 kutoka Shehiya za Kidimni, Ubago pamoja na Koani.

Aidha, Mis Soon Choi akisoma Risala ya Washirika wa Maendeleo , alisema mafanikio ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho yanatokana na mashirkiano makubwa waliyoyapata kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kati Unguja pamoja na Wizara ya Afya, Ustawi wa jamii, Wazee, Jinsia na Watoto.

Alisema Serikali ya Korea Kusini itaendeleza mashirkiano kati yake na Zanzibar, sambamba na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.