Habari za Punde

Kadhaa, Kadhaa wa Kadhaa.

Na.Adeladius Makwega - DODOMA.

Msomaji wangu, leo hii nakuletea picha hiyo juu ya ndugu zangu wanne; Biligita (57), Demetria (52), Bernadeth (56) na Corinelia (amefariki) wote ni Binti Makwega iliyopigwa mwaka 1985 Mbagala Sabasaba Temeke-Dar es Salaam wakiwa mabinti wadogo sasa ni watu wazima.

Mimi siku hiyo sikuwepo lakini kwa desturi ya maisha yetu ya Tanzania ya wakati huo picha zilipigwa sana wakati wa wa sikukuu tu, sivyo kama ilivyo sasa, kwa kuwa wapiga picha walipata wasaa wa kupata wateja wengi siku za sikukuu kuliko siku nyengine yoyote.

Ndugu zangu hao wote walisoma shule ya msingi Mbagala tangu darasa la kwanza hadi la saba na mimi nikiwashuhudia wakisoma shule hii kongwe ya msingi. Umbali kati ya nyumbani kwetu na shule hii ni kama kilomita tatu. Wakipita njia ya Bonde la shamba la Jaji Mstaafu Kimicha ambalo aliuliziwa na Bibi Sela (Bibi Sara) Bibi mmoja mzungu  ambaye aliondoka kurudi kwao ughaibuni muda mfupi baada ya uhuru Tanganyika.

Kwa hiyo shule ya msingi Mbagala ukijumlisha waliosoma wengi kutoka kwetu baba, mashangazi zangu hao, sisi watoto wao wote wa kike na wakiume, tulikuwa wengi mno idadi inakaribia kati ya watu 20-30 wa ukoo mmoja kwa kipindi cha mfuatano tafauti tangu mwaka 1950 na hadi sasa ikiongezeka zaidi.

Zipo koo zingine nyingi kama vile Zame, Makuka, Mkundi(Kizuiani), Mkundi (Sabasaba), Linje, Ngunga, Ungaunga na Mangaya zikiungana na akina Makwega wakisoma wengi shuleni hapo, huku zikiwepo koo nyingine nyingi zilizokuwa na watu wachache wachache shuleni.

Tukiwa tunakwenda shuleni tuliongozana makundi makundi, yawe ya watu watano  watano huku wale wadogo wakiongozwa na waliokuwa wakubwa iwe wakati wa kwenda  shuleni au wakati wa kurudi nyumbani.

Njia ya mkato ya Pori la Jaji Kimicha (Kwa Bibi Sela) ililokuwa na nyoka, chatu kadhaa huku adui mwingine akiwa binadamu (vijana) wakorofi njiani.

Vijana wakorofi walikuwa pia hata wanafunzi wenzetu ambapo mkigombana shuleni ugomvi huo unaweza kuhamishiwa wakati wa kurudi nyumbani. Kwa hiyo mkiwa njiani kutokea ndundi (ngumi) ni jambo la kawaida mno.

Kwa safari hizo za kwenda na kurudi zilikuwa za kila siku jumatatu hadi Ijumaa tangu darasa la kwanza hadi la saba, huku katika familia yetu wale wakubwa wakimaliza shule na kuanza maisha au kuendelea na masomo.

Safari hizo za kwenda na kurudi shule, mimi nikiwa mdogo zilikuwa zikiongozwa na shangazi yangu aliyefahamika kama Biligita Makwega (wa kwanza mkono wako wa kushoto msomaji wangu katika picha hiyo). Yeye alikuwa na mwili uliojengeka sana, akiwa na pumzi, akiwa ana nguvu za kuwadhibiti ipasavyo wale waliokuwa wakituletea fujo njiani, wawe wanafunzi au wanakijiji kama wanaume au mwanamke cha mtema kuni  walikiona kutoka kwa Biligita.

Mnapokuwa shuleni mnaweza kusikia kelele za kilio, ukiwa unasoma unatega sikio kilio hicho si cha ndugu yenu? Kama si cha ndugu yenu mnawajulisha wenye ndugu yao ili wafuatilie kulikoni?

“Huko ndugu yenu anapigwa! ”  Hiari yao,kwenda kufuatilia au la.

Kikiwa cha ndugu yenu wote mnatoka kwenda anapolia ndugu yenu, kujua kulikoni? Wakati wa kutoka darasa unaweza kuulizwa, ehee, we Makwega, unakwenda wapi?

“Mwalimu nakwenda kujisaidia.” Tulijibu kwa hekima.

Hapo mwalimu lazima atoe ruhusa, ukiona mwalimu hataki basi unaweza hata kuigiza kuwa umebanwa sana, hapo ruhusa inatolewa na kukimbilia kwenye kilio.

Huko mnaweza kukutana watatu, wane n ahata zaidi, mmoja wenu atauliza alichokifanya ndugu yenu hadi anaadhibiwa? Kama hali ikiwa ngumu shangazi Biligita atajulishwa.

Kama adhabu ni ya haki mtaachana na tukio hilo na kurudi kusoma. Kama tukio si haki, kwa hekima tu bila fujo, jambo hilo litaamuliwa kwa haki iwe kwa mkuu wa shule au kamati ya shule maana wenye shule ni kamati inayosimamiwa na wazazi wetu.

Kwa nini ninayasema haya ? Tunasema kuwa sisi sote ni ndugu, Je linapomkuta baya miongoni mwetu ni kilio chetu sote? Kama kweli sisi sote ni ndugu, Je mwanakwetu unafahamu sauti ya kilio cha ndugu yako anapokuwa na shida ? Je kilio hicho kina mawimbi gani ? Je ya juu au chini? Je unakimbilia na kwenda kuuliza amefanya kosa gani? Je adhabu hiyo anayopewa ni ya haki? Je wewe unafanya nini katika hilo? Umeijulisha kamati ya shule ambayo ndiyo yenye shule yetu? Kama umeijulisha kamati imekaa kimya mnachagua kamati nyingine. Au walimu wanafanya watakavyo? Kama walimu wanafanya watakavyo mnawakataa kwa sababu  kadhaa, kadhaa wa kadhaa.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.