Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Afunga Mafunzo ya USAID.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitoa nasaha zake kwa Viongozi, Vijana na Wadau mbali mbali wa Maendeleo wakati akifunga Mradi wa Inua Vijana Hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar ambapo amewataka Wanufaika wa Mradi huo kuyafanyia kazi yote waliyojifunza  na kuutumia ujuzi waliyoupata ili kujikwamua Kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amelitaka Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kuendelea kuunga Mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Miradi mbali mbali ili kusaidia kukuza Uchumi wa Mtu Mmoja Mmoja na Taifa kwa Ujumla. 

 

Mhe. Hemed ametoa Kauli hiyo wakati akifunga Mradi wa Inua Vijana uliofadhiliwa na USAID hafla iliofanyika Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar. 

 

Amesema kuna haja ya kuelekeza nguvu kwa kuwekeza katika Sekta ya Uchumi wa Buluu na kuwawezesha Wanawake ili kuweza kujikwamua kimaisha.

 

"Natoa wito kwa Shirika la Maendeleo la Marekani USAID kuona haja ya kupanua wigo wa uhusishaji wa Miradi inayojumuisha Uchumi wa Buluu, kuwapa kipaumbele Wanawake katika upatikanaji wa Ruzuku na kujenga mnyororo wa thamani kwenye sekta ya Hoteli na kuhakikisha Chakula kinazalishwa na kuuzwa ndani na nje ya Nchi" amesema

 

Mhe. Hemed ameeleza kuwa hatua waliochukua Shirika hilo ni ya kupigiwa mfano ambapo wanaenda sambamba na Programu za Ajira chini ya Uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo  kuwawezesha Vijana kujiajiri ili kupunguza utegemezi kwa Serikali. 

 

Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeweka Mazingira mazuri ya kuwawezesha Vijana kuwa wabunifu na kuweza kujiajiri na imetenga Jumla ya Shilingi Bilioni Sita nukta Nne (6.4)  kwa ajili ya uwekezaji wa Programu ya Vijana.

 

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina Malengo ya kuweka Mazingira mazuri na endelevu kwa Vijana ili waweze kujiimarisha kiuchumi na Kijamii kwa kuwapatia Mafunzo mbali mbali ya kitaaluma waweze kuwa wabunifu na kujiajiri wenyewe sambamba na kujipatia kipato chenye tija kwa kujiendesha na maisha yao ya kila siku. Kwa Mwaka huu 2022/2023 Serikali imejipangia Programu hii Jumla ya Shilingi Bilioni 6.4 kwa ajili ya kutekeleza Shughuli zake" amesema

 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa Maendeleo ili kutumiza Dira na Dhamira ya kukuza Uchumi wa Zanzibar kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050.

 

Pamoja na Mambo mengine Mhe. Hemed amechukua fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Marekani kwa kuipa umuhimu Mkubwa wa kuanzisha Programu ya kuinua Vijana Tanzania na kueleza furaha yake kuona miradi  mengine waliyoipanga katika Sekta mbali mbali ikiwemo Kilimo kwa kuwekeza Dola Bilioni Tano za Kimarekani.

 

Aidha Mhe. Hemed amewaasa Wanufaika wa Mradi huo kuendelea kuutumia ujuzi, maarifa na Stadi walizopatiwa katika kujiajiri ili kupunguza kiwango cha Umasikini Nchini.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha  Vijana wenye sifa wanapatiwa Mikopo ili kujiwezesha na kuitaka Wizara hiyo kukaa pamoja na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Biashara kuandaa mpango kazi wa kuwatafutia soko la uhakika hasa katika Mahoteli Nchini.

 

‘’Serikali imekusudia kuibadilisha Zanzibar Kiuchumi na Vijana ni moja kati ya makundi tuliyolenga kuyaangalia sitaki kusikia Vijana wanasumbuka katika suala la Mikopo fedha zipo vijana jitokezeni ili mufanikiwe  Wizara simamieni Vijana wafanyekazi’’ Mhe. Hemed

 

Kwa upande wake Kaimu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Simai Mohamed Said ameeleza kufurahishwa kwake kwa Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania kuichagua Zanzibar kuwa miongoni mwa Nchi zilizonufaika na Mradi huo.

 

Aidha ameeleza kuwa Wizara itasimamia Fursa mbali mbali za Soko la Bidhaa za Chakula zinazozalishwa na vijana wanaowezeshwa na Mikopo mbali mbali ili kuwarahisishia usambazaji wa Bidhaa zao.

 

Nae Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Mhe. Donald Wright ameeleza kuwa Mradi huo umeelekezwa kwa kuwapatia mafunzo Vijana wa Tanzania pamoja na upatikanaji wa vifaa kwa wajasiriamali baada ya Mafunzo. 

 

Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Watu wa Marekani itaendeleza Mashirikiano yake  na Tanzania katika miradi mbali mbali itayosaidia kuinua Uchumi wa Nchi.


………………………..

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

02 /08/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.