Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Akutana na Kuzungumza na Uongozi wa TIRA.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutambua Mchango wa Mashirika ya Bima katika Kukuza Uchumi wa Nchi pamoja na kusaidia Wananchi wanapokutwa na Majanga.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Kauli hiyo alipokutana na Uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima Tanzania (TIRA) pamoja na kukabidhi Miongozo ya kiutendaji Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar. 

 

Amesema Serikali inaridhishwa na mienendo ya Mashirika hayo katika kusaidia Jamii hasa wanapokutwa na Majanga hatua ambayo inasaidia kupunguza athari zinzojitokeza wanapokumbwa na Maafa.

 

Mhe. Hemed amefurahishwa na uwepo wa Mpango wa utekelezaji wa Mamlaka hiyo na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia utekelezaji wa Mpango huo kwa vitendo.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa mbali na uwepo wa Sheria mbali mbali Nchini bado  wadau wa Bima wana haki ya kuishauri Serikali kurekebisha  Sheria ili kuendana na hali zao za kiutendaji kwa lengo la kuboresha Huduma zao ziwafae zaidi Wananchi. 

 

Sambamba na hayo ameeleza kuwa bado Jamii inahitaji Elimu ya ziada kuhusiana na Umuhimu wa kukata Bima hivyo, ameutaka Uongozi huo kuongeza juhudi za kuwafikia Wananchi hasa Wawekezaji, Wafanyabiashara na Makundi mbali mbali ili kujiunga na Huduma hizo.

 

Kwa upande wake Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Abdallah Saqwere  amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Mpango waliomkabidhi umejumuisha suala la Ajira, Mfumo wa usambazaji Bima Kidigitali pamoja na Bima ya Takaful.

 

Aidha Dkt. Daqwere ameeleza kuwa TIRA tayari wameshawakaribisha Wawekezaji kuja kuwekeza katika Takaful pamoja na kueleza Azma yao ya kuhamasisha ukataji wa Bima katika maeneo ya Kijamii ikiwemo Masoko, Bidhaa zinazoingia Nchini na maeneo mengine mbali mbali.


Wakati wa Mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Mhe. Donald Wright Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar ambapo walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbali mbali ya kuendeleza uhusiano baina ya Nchi mbili hizo.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.