Habari za Punde

Waziri Mhe.Lela Alitembelea Mradi wa Kuwarudisha Watoto Skuli Unaofadhiliwa na QATAR na UNICEF na kuangalia hatua ya ujenzi wa madarasa ya wanafunzi walioacha kusoma kwa sababu mbalimbali

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Mhe.Lela Mohmmed Mussa, amesema hajaridhishwa na utendaji kazi wa walimu wa Skuli ya Bububu ‘B’ kutokana na kushindwa kuwajibika kwa mujibu wa miongozo ya kiutumishi serikalini.

Akizungumza katika ziara ya kushitukiza katika skuli hiyo, alisema, hatua hiyo inasababisha walimu hao kutojua changamoto za wanafunzi zinazowakabili wakati wakiwa skuli na badala yake husabbaisha kupata matokeo yasiyoridhisha katika mitihani yao ya Taifa.
Amesema, walimu wamekuwa wakenda skuli bila ya kuingia na miongozo wakati wa kufundisha jambo ambalo linaonesha dhahiri kuwa hawana sifa wala uwezo wa kufundisha.
Aidha alisema kuwa, walimu wa skuli hiyo wamekuwa wakifanya makosa ya wazi kwani wamekuwa hawatendei haki wanafunzi wao.
“Haiwezekani wewe mwalimu mwaka mzima unaingia darasani ila ya muongozo, sikubaliani na walimu hawa mimi na sijaridhishwa na utendaji wao wa kazi” .
Hivyo, alimuagiza Mkurugenzi wa Elimu Sekondari kwa Katibu Mkuu wa Wizara kuwa walimu wa skuli hiyo wamekosa sifa za kuwa walimu na kuwaandikia barua ya onyo na hatua za kiutumishi zichukuliwe dhidi ya walimu hao.
Sambamba na hayo, amemuagiza, Katibu Mkuu, kumteuwa Mwalimu Mkuu wa skuli ili kuona mabadiliko yanatokezea katika skuli hiyo, pamoja na kusema kuwa hajaridhishwa na utendaji wa kazi wa kaimu mwalimu mkuu wa skuli hiyo kwa sasa jambo ambalo limesababisha kutokea kwa changamoto alizokutana nazo.
Wakati huo huo, Waziri Lela, alitembelea mradi wa kuwarudisha watoto skuli unaofadhiliwa na QATAR na UNICEF na kuangalia hatua ya ujenzi wa madarasa ya wanafunzi walioacha kusoma kwa sababu mbalimbali.
Amesema, wafadhili hao wamewekeza fedha nyingi sana hivyo ni vyema walimu kusimamia mradi huo na kuona lengo linafikiwa kama ilivyokusudiwa.
“Wafadhili wetu wamewekeza fedha zao kuona watoto wetu wanarudi skuli, hivyo walimu wenzangu tulisimamieni hili ili lengo liweze kufikiwa na tija iweze kupatikana” amesema.
Nao, baadhi ya Walimu wamesema, baadhi ya changamoto zilizosababisha watoto hao kuacha skuli ni pamoja na ugonvi wa kifamilia na umasikini, jambo ambalo linasababisha wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo.
Hivyo, wamewaomba wazazi wanapokuwa na sitofahamu kutowashirikisha watoto wao kwani wanasababisha watoto wao kukosa masomo na badala yake hufanya kazi zilizokuwa sio rasmi ikiwemo kujiingiza katika ajira za utotoni.
Skuli zilizotembelewa na uongozi wa Wizara ya Elimu ni skuli ya msingi Chumbuni, Fukuchani, na skuli ya msingi Mahonda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.