Habari za Punde

DKT.DIMWA-AKEMEA VIKALI WANASIASA WANAOHUBIRI UTENGANO

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed (Dimwa),amekemea vikali kauli zisizofaa za kuhubiri utengano,upotoshaji na kubeza maendeleo yanayopatikana chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK), zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa.

Alisema wanasiasa hao wanatakiwa kujitathimini juu ya mwenendo wao unaolenga kuchafua thamani,tija na mafanikio yaliyopatika chini ya mfumo huo.  

Hayo aliyaeleza katika mahojiano na Kituo cha Radio ya Assalam FM, alisema maridhiano hayo ya kisiasa hayakutokea kwa miujiza bali yaliasisiwa na Chama Cha Mapinduzi.  

Dkt.Dimwa, alisema  Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Ibara ya 9(a) imeahidi katika kipindi cha miaka mitano kazi kubwa itakayofanywa na CCM ni kuimarisha maridhiano, kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Alieleza kwamba kutokana na mkataba huo wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM uliofungwa baina ya Wananchi na Chama Cha Mapinduzi umeeleza wazi umuhimu wa maridhiano hayo yanayotakiwa kuenziwa,kuheshimiwa na kulindwa kwa gharama yoyote.

“Wapo baadhi ya wenzetu wameanza kutoa kauli zisizofaa juu ya mfumo huu wakidai haufai,niwakumbushe kuwa haya sio matakwa ya mtu mmoja ama kundi fulani bali ni maridhiano yaliyopo katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.”, alifafanua Dkt.Dimwa.

Alieleza kwamba kazi ya kulinda maridhiano hayo imeendelea kutekelezwa vizuri na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inakuwa miongoni mwa nchi za visiwa zilizoendelea kiuchumi.

Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, alieleza wazi kuwa chini ya uongozi wake hatofumbia macho  vitendo na kauli za kuingiza nchi katika machafuko na badala yake atachukua hatua kali kupitia utaratibu wa Kisheria.

Pamoja na hayo alisema kama kuna viongozi na wanasiasa wasioridhika na mfumo huo waitishe  mazungumzo kwa lengo la kujadili na kupata suluhu na ufumbuzi wa kudumu.

“Najipanga hivi karibuni kuwaita vyama vyote vya upinzani tukae pamoja tuzungumze kwa lengo la kulinda tunu hii ya maridhiano ya nchi yetu”.alieleza Dkt.Dimwa.

Kupitia mahojiano hayo alisema, kazi yake kubwa ni kuhakikisha anatekeleza matakwa ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo jipya la 2022 ibara ya 5 (1) ya kuhakikisha Chama kinashinda uchaguzi wa Dola.

Alisema kazi nyingine ni kuwasimamia Wabunge,Wawakilishi na Madiwani watekeleze ahadi walizotoa kwa wananchi ili kumaliza changamoto zilizopo majimboni.

Pamoja na hayo alitaja vipaumbe vyake vitano vitakavyo muongoza katika utendaji wake kuwa ni kutekeleza majukumu yake kwa kasi yenye viwango.

Kipaumbe cha pili alisema ni kutekeleza kwa vitendo dhana ya siasa na uchumi kwa kuhakikisha anabuni miradi ya yenye tija itakayosaidia kujiimarisha kiuchumi.

Alisema kipaumbele cha tatu ni elimu kwa kuhakikisha watendaji,viongozi na wanachama wanapata fursa za kusoma na kujengewa uwezo kitaaluma.

Aidha alikitaja kipaumbe cha nne kuwa ni kuhakikisha chama kinarudi kwa wanachama wake kwa kuwasimamia watendaji na viongozi kushuka ngazi za chini kusikiliza na kuratibu changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi wake.

Kipaumbele cha tano alieleza kuwa ni kuwajengea uwezo wanawake nchini ili wapate uwezo wa kugombea majimbo kwani wamekuwa wakipambana na changamoto nyingi zikiwemo rushwa ya fedha,kutishwa na kukatishwa tamaa.

Pamoja na hayo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu kwani ndio chimbuko la maendeleo endelevu ya Zanzibar katika nyanja za kiuchumi,kisiasa,kijamii na kidiplomasia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.