Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Amekutana na Kuzungumza na Waziri wa Hijja na Umra wa Saudi Arabia

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Hijja na Umra wa Saudi Arabia Mhe. Dkt. Tawfyq Al - Arabian katika Ofisi za Wizara hiyo Mjini Makkah Nchini Saudi Arabia. 

Mhe. Hemed ameongozana Balozi wa Tanzania Nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Jabir Mwadini,  Katibu Mtendaji Kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Sheikh Abdallah Talib ambae ni Mwenyekiti wa Afisi Kuu ya Hijja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Biitha). 

Katika mazungumzo yao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru Serikali hiyo kwa kuendeleza mashirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendeleza mashirikiano kwa faida ya pande zote mbili

Sambamba na hayo Alhajj Hemed ameishukuru Serikali ya Ufalme wa Saudi Arabia kupitia Shirika la Ndege la Saudi  airline kwa kuanzishia Safari za Moja kwa moja kutoka Jeddah kuelekea Dar - es - Salaam Tanzania.

Aidha Mhe. Hemed ameiomba  Serikali ya Saudi Arabia kupitia Shrika la Saudi Airline  kufikikisha huduma zake  Zanzibar  ikizingatiwa  kuwa Zanzibar ina Idadi kubwa ya Mahujaji.

Kwa upande wake Waziri wa Hijja na Umra wa Saudi Arabia Mhe. Dkt. Tawfyq Al - Rabiah amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka Sera nzuri na juhudi zake za kuwatumikia watanzania hatua ambayo inasaidia kuwaletea maendeleo wananchi hao.

Aidha amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuiletea Maendeleo Zanzibar na kusifu kuwepo mazingira mazuri ya kibishara na vivutio vya kitalii  ambapo yeye binafsi amejiinea wakati alipofika Zanzibar kujionea vivutio mbali mbali ikiwemo fukwe nzuri, urithi wa Mji mkongwe, mashamba ya Viungo (Spices)  pamojana ukarimu wa wananchi wake.

Nae Balozi wa Tanzania Nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Jabir Mwadini  ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa kuanzisha utaratibu wa kutumia mawakala katika kusafirisha Mahujaji jambo ambalo limeiwezesha Afisi Kuu ya Hijja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Biitha)  kusajili Idadi kubwa ya Mahujaji kutokana na kupunguwa kwa gharama.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR) 28 Machi, 2023. Makkah.






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.