Habari za Punde

Mbunge wa Jimbo la Amani Mhe. Abdul - Amesema Dhamira Yake ni Kufanya Mapinduzi ya Kimaendeleo Ndani ya Jimbo la Amani

MBUNGE wa Jimbo la Amani Mhe.Abdul Yussuf Maalim(wa tatu kutoka upande wa kulia) akiwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe.Rukia Mapuri(wa pili kutoka upande wa kushoto) na madiwani wa wadi za jimbo hilo wakimsikiliza mwananchi anayetoa ufafanuzi juu ya ukosefu wa huduma ya maji baada ya kuibiwa mashine katika kisima cha eneo hilo.

Na.Mwandishi Wetu --ZANZIBAR.

MBUNGE wa Jimbo la Amani Zanzibar Mhe.Abdul Yussuf Maalim,amewasihi wananchi wa jimbo hilo kutunza,kulinda na kuthamini miundombinu ya maji safi na salama.

Nasaha hizo amezitoa kwa wakati tofauti katika ziara yake ya kukagua na kutathimini changamoto zinazoikabili sekta ya maji ndani ya jimbo hilo.

Alisema kila mwananchi katika maisha yake ya kila siku anahitaji huduma ya maji safi na salama hivyo ni lazima jamii ishiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya maji isihujumiwe.  

Mhe.Abdul, alieleza kuwa kupitia ziara hiyo wamebaini uharibifu mkubwa wa miundombinu ya maji hali inayosababisha baadhi ya shehia kutopata huduma hiyo kwa wakati.

Aliwasihi wananchi wa jimbo hilo washirikiane kulinda miundombinu hiyo na rasilimali zingine zisiibiwe kwani madhara yake yanawaathiri wananchi wa maeneo husika.

“ Wakati nikiomba kura kwa wananchi wa jimbo hiki niliahidi kumaliza changamoto ya upungufu wa maji katika shehia zote,kwa hatua ya kwanza nimetembelea jimbo lote leo kukagua,kutahimini na kuratibu changamoto hii ya ukosefu wa maji ili kujua ukubwa wa tatizo.

Niliomba kazi hii kwa hiari yangu nipo tayari kukutumikieni kwani dhamira yangu ni kufanya mapinduzi ya kimaendeleo ndani ya jimbo hili, huku nikishirikiana na viongozi wenzangu kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.”, alisema Mbunge huyo Abdul.

Katika maelezo yake Mhe.Abdul,alisema atatekeleza kwa vitendo falsafa ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha anaimarisha mbiundombinu ili huduma za maji zipatikane wakati wote.

Pamoja na hayo alisema atahakikisha anaimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwani unakaribia mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao wananchi wanahitaji huduma hiyo kwa wakati.

Naye Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe.Rukia Omar Mapuri,alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini katika kulinda mali za umma zisiharibiwe ambapo gharama zinazotumika zinatokana na fedha za mfuko wa jimbo hilo.

 “Nakuombeni wananchi wenzangu tuishirikiane katika masuala mbali mbali ya kijamii ili jimbo letu liwe la kuigwa kwa maendeleo kwani sisi viongozi wenu tupo tayari kukutumikieni usiku na mchana.”,alisema Rukia Mapuri,

Rukia, alieleza kuwa wanajipanga kuingiza fedha nyingi  katika miradi ya maendeleo ya jimbo  ili kuongeza ufanisi katika sekta za elimu,afya,maji,barabara za ndani,vikundi vya ujasiriamali na michezo na burudani.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wananchi wa jimbo hilo waliwapongeza viongozi hao kwa maamuzi yao ya kukagua maeneo mbali mbali yenye changamoto ya upungufu wa maji.

Naye Mkaazi wa mtaa wa Kilima hewa juu Ndg.Khadija Salim,aliwashauri viongozi hao kuwa baada ya kufanya matengenezo ya miundombinu hiyo waweke viongozi wenye uwezo wa kusimamia na kufuatilia harakati zote za utoaji wa huduma ya maji kwa kila kisima.

Ziara hiyo iliyofanyika leo Machi 4,mwaka 2023,ikiwa na Mwakilishi Mhe.Rukia Mapuri,Madiwani wa Wadi za Jimbo hilo pamoja na Mbunge wa jimbo hilo Mhe.Abdul Yussuf ambayo ni ziara yake ya kwanza toka achaguliwe kuwa mbunge aliyeshinda  kwa kura 4, 242 sawa na asilimia 84.1 akifuatiwa na mgombea wa ACT Wazalendo, Mohamed Khamis Mohamed aliyepata kura 728 sawa na asilimia 14.4.

Uchaguzi huo ulijumuisha vyama 14 vya siasa, kufuatia kifo Cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mussa Hassan Mussa kilichotokea Oktoba mwaka 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.