RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi aliiasa jamii kuendelea kuwajengea uwezo vijana
ili kukuza jamii yenye maadili mema na hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu (S.W.)
Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye halfa ya
mashindano ya Quran tukufu kwa njia ya
Tartil yaliyofanyika ukumbi wa Golden
Tulip, Uwanja wa ndege Zanzibar.
Alisema kumekuwa na mporomoko wa maadili na kupotea
kwa sehemu kubwa ya mila na silka za Wazanzibari, hivyo alieleza kupitia
utaratibu wa kuwahifadhisha vijana Quran tukufu ni njia ya kuzalisha viongozi
bora wa baadae wakiwemo Masheikh na Maulamaa.
Alisema hatua hiyo pia inahamasisha jamii juu ya
kuendelea kukisoma kitabu kitukufu cha Qur’an ambacho ndani yake kuna faida
nyingi zikiwemo kukisoma, kukisomesha na kukihifadhi.
Katika halfa hiyo, pia Al hajj Dk. Mwinyi alitoa
zawadi ya shilingi milioni moja kwa kila
mshindi, kwa washindi watano wa mwisho ikiwa ni zawadi za ushiriki wao kwenye
mashindano hayo, pia aliitaka jamii iendeleze kuhamasisha vijana wengi kwenye
mashindano yajayo ili kukisoma vyema kitabu kitakatifu cha Qur’an.
Vile vile, Al hajj Dk. Mwinyi
alitumia fursa hiyo kuziomba sekta binafsi kuungana na sekta za umma kutoa
mapema mshahara wa mwezi Aprili mwaka huu baina ya leo (Aprili 19) na kesho
(Aprili 20) ili kuwapa muda wa
kutosha wafanyakazi wao kwa maandalizi ya sikukuu ya Eid Fitri inayotarajiwa
hivi karibuni.
Alisema maombi hayo yamekuja kufuatia maagizo
aliyoyatoa Apirili 16 mwaka huu kwa taasisi zote za umma kuwapa mapema mshahara
wa mwezi huu watumishi wa umma ili wafurahie vizuri sherehe za sikukuu, baada
ya Mfungo mtukufu wa Ramadhan.
Rais Dk. Mwinyi alisema baada ya maagizo yake
alipokea maombi mengi kutoka kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ili nao wafaidike
lakini kwa vile hana mamlaka na sekta binafsi, aliziomba sekta hizo waridhie
maombi yake na wawape mishahara wafanyakazi wao baina ya leo na kesho.
Akizungumza kwenye halfa hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman
alisifu juhudi za Rais Al hajj Dk. Mwinyi katika kuungamkono na kuendeleza
masula ya khairati nchini.
Alisema tokea kunza kwa Mfungo mtukufu wa Ramadhan,
Al hajj Dk. Mwinyi amefanikiwa kufutarisha nchi nzima kwa mikoa yote ya Unguja
na Pemba, aidha, aleleza taifa limemshuhudia akishiriki ibada za sala za pamoja
na wananchi wake zikiweo Ijumaa na Taraweikh kwa kipindi chote cha swaum kwa maeneo
mbalimbali ya mjini na vijijini.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa
huduma za kibenki kutoka Benki kuu ya watu wa Zanzibar (PBZ), Said Muhamed
Said, alisema benki hiyo haiko nyuma kwenye kujikita na masuala ya jamii ili
kuendelea kuwa karibu na wateja wake. Alisema PBZ inawajibu wa
kushirikiana na Serikali kwenye kupata vijana wenye maadili mema pamoja na
kuiunga mkono serikali kukuza na kuendeleza maadili ya vijana.
PBZ ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo waliiomba
jamii kuendelea
kuitumia ili na wao waendelee kuungamkono shughuli za jamii.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazi Zanzibar
(ZBC), Salum Ramadhan Abdalla Shaaban ambao ni waratibu wa mashindano hayo kwa
kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, alisema mashindano hayo yalianza
mwaka jana baada ya kuzaliwa wazo na ZBC kabla ya kuliwasilisha Wizara ya
Habari ambayo mafanikio yake yamekua endelevu hadi sasa.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirika la
Utangazaji, Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, yaliibua
washindi watatu, mshindi wa kwanza alizawadiwa gari aina ya Alphad, mshindi wa
pili bodaboda na mshindi wa tatu fedha taslimu, shilingi milioni mbili.
IDARA YA MAWASILINO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment