Habari za Punde

Mhe Othman akutana na kufanya mazungumzo na Balozi mdogo wa Uingereza nchini Tanzania

 


Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman , amesema kwamba kuanza kwa vikao vya Kamati ya pamoja ya Maridhiano ya Kisiasa kati ya Chama cha ACT -Wazalendo na Chama cha Mapinduzi (CCM), ni hatua muhimu ya kutia moyo na ya kuleta matumaini ya kuwepo na kuendelea  mjadala  wa masuala mbali mbali yanayohusu mustakabali mwema wa Zanzibar .

Mhe. Othman ameyasema hayo nyumbani kwake Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, alipokutana na Balozi mdogo wa Uingereza nchini Tanzania Rick Shearn, aliyetaka kujua pamoja na mambo mengine maendeleo ya Kamati hiyo ya Pamoja iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Amesema kwamba hivi sasa Kamati hiyo imeanza vikao vyake kwa kujadili maeneo na agenda  muhimu  na makhususi  na namna  ya utaratibu bora utakaotumika katika kuyajadili masuala muhimu kwenye agenda hizo ili kuweza kufikia muafaka kwa malengo yaliyokusudiwa ya mustakabali wa Zanzibar na watu wake.

Aidha Mhe. Othman amesema anaamini kwamba katika vikao hivyo vya awali maeneo yote muhimu yanayohitaji kufanyiwa mabadiliko na mageuzi makubwa yameainishwa kwa kuwasilishwa na kujadiliwa  kwa pamoja katika kutafuta maslahi bora ya Zanzibar na  watu wake.

Mhe. Makamu amefahamisha kwamba kuwepo kwa hatua hiyo ni fursa muhimu kwa Zanzibar katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa 2025 katika kufanya mabadiliko na mageuzi yanayotarajiwa na wananchi wa Zanzibar katika kuweka matumani ya mustakabali wa nchi yao.

Amesema majadiliano hayo ya awali yamegusa katika maeneo muhimu yote likiwemo suala la Mageuzi na mabadiliko  katika masuala ya Uchaguzi ikiwemo Tume inayosimamia uchaguzi ili kuifanya kuwa taasisi imara kwa maendeleo na mustakabali mwema wa Zanzibar.

Amefahamisha kwamba agenda ya mausuala ya uchaguzi linaendelea kama jambo muhimu katika misingi ya mjadala huo kwa kuwa unalenga maisha ya wazanzibar, biashara kwa Zanzibar, pia ni uwekezaji kwa maendeleo ya nchi.

Amesmea kwamba kwamba Zanzibar inahitaji uwekezaji na wawekezaji wanahitaji kuwekeza fedha zao katika eneo salama na lenye utulivu ili waweze kufanya biashara na wageni kutembea Zanzibar kupitia sekta ya utalii.

Amesema kwamba masuala mengi yanagusa mambo muhimu ikiwemo pia mabadiliko katika sekta za umma na kuwepo uwajibikaji na utawala wa sheria yameainishwa kwa kuwa ni mambo yatakayosaidia kuondosha udhaifu katika maeneo mbali mbali ya sekta za umma  ili kujenga maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Akizungunzia suala la Katiba Mpya , Mhe. Othman amesema kwamba hilo ni suala la Muungano, lakini linagusa maendeleo ya masuala kadhaa ya Zanzibar moja kwa moja ambapo yapo masuala mengi yanayohitaji kufanyiwa mageuzi katika usimamizi na uendeshaji wake ikiwemo suala la haki jinai na uchaguzi wa wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Balozi Mdogo wa  Uingereza nchini Tanzania  Rick Shearn alitaka kufahamu iwapo suala la Katiba mpya ya Jahuri ya Muungano wa Tanzania pia linaweza kuathiri mustakabali wa Zanzibar  katika uchaguzi ujao wa 2025 na utekelezaji wa msuala mbali mbali  ikiwemo  uchaguzi wa Zanzibar.

 

Mwisho.

Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar

Agosti 10, 2023

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.