Habari za Punde

Waziri Mhe.Rahma Kassim Azungumzia Mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar Katika Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi  Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali akitoa taarifa kuhusiana na Mapinduzi ya sekta ya Ardhi na maendeleo ya makaazi kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi, huko Karume House

Mwandishi wa habari shirika la magazeti ya serikali Mwanajuma Juma akiuliza swali kwa Waziri wa Ardhi na maendeleo ya makaazi  Mhe. Rahma Kassim Ali wakati akiwasilisha taarifa ya Mapinduzi ya sekta ya Ardhi na maendeleo ya makaazi kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi, huko Karume House.

Waziri wa Ardhi na maendeleo ya makaazi  Mhe. Rahma Kassim Ali akitoa taarifa kuhusiana na Mapinduzi ya sekta ya Ardhi na maendeleo ya makaazi kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi, huko Karume House

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR

Na.Sheha Sheha -Maelezo Zanzibar.- 20-12-2023.

Waziri Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Rahma Kassim Ali amesema Serikali inaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kufuata Sheria za ardhi ili kuepukana na migogoro isiyo ya lazima kwa wananchi.

Waziri Rahma amesema hayo leo katika Ukumbi wa ZBC, Karume House. wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mikakati, malengo na mafanikio ya Wizara hiyo Kuelekea madhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kupitia njia mbali mbali juu ya umuhimu wa kufuata Sheria za ardhi ili kuepukana na vichocheo vinavyopelekea migogoro ya ardhi isiyo ya lazima  Nchini.

Amesema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi inaendelea kuweka Mifumo ya kidigitali ili kurahisisha upatikanaji huduma kwa jamii na kuziba mianya ya rushwa na upotevu wa mapato Nchini.

Amesema, Serikali imekamilisha uthamini wa mali kwa ajili ya ulipwaji wa fidia ili kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo Miradi inayosimamiwa na Shirika la Umeme, Mamlaka ya Maji, Ujenzi wa Masoko makubwa, Ujenzi wa Hospitali kubwa za Mikoa na Wilaya, Ujenzi wa Barabara na upanuzi wa viwanja vya Ndege Unguja na Pemba.

Amefahamisha kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wa uhaulishaji ardhi na kufanikiwa kupunguza muda wa huduma za uhaulishaji wa ardhi kutoka siku 30 hadi siku 15 baada ya  taratibu na vielelezo kukamilika ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Waziri Rahma amesema Serikali imeanzisha Kamisheni  hiyo yenye Lengo la kusimamia masuala yote ya ardhi pamoja na kuziunganisha taasisi zinazosimamia matumizi na maendeleo ya ardhi ili kuleta usimamizi bora Nchini.

Amefahamisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ikiwemo Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Ardhi, Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi pia inaendelea kupanga Mipango ya miji midogo  midogo kwa Unguja na Pemba ili kuitumia Ardhi kwa ufanisi.

 

“Serikali imefanikiwa kupima ardhi ya akiba katika zoni tano pamoja na kukamilisha upangaji wa maeneo ya Nungwi, Mkokotoni, Chwaka, Dunga, Mahonda na Makunduchi.” Alisema Waziri Rahma.

Hata hivyo amesema Serikali imeweka Sera na Sheria mbali mbali za kusimamia masuala ya Uwekezaji katika Sekta miliki na kuruhusu wafanyabiashara kuingiza vifaa vya ujenzi wa nyumba pamoja na kutoa  Msamaha wa Kodi kwa Wawekezaji ili kuwasaidia wananchi kupata Makazi bora kwa urahisi.

Hafla hiyo ikiwa ni muendelezo wa mahojiano baina ya Mawaziri wa Wizara mbali mbali na Waandishi wa Habari katika kuelezea maendeleo, malengo na mafanikio ya Wizara, kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.