Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria katika hafla ya Mkutano na Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita Kuhusiana na Taarifa ya Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari linalotarajiwa Kufanyika Tarehe 18/09/2024 katika Uwanja wa Mpira Misuka Mahonda Kaskazini Unguja ,ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa Kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi na Ujumbe wa Mwaka Huu ni "Tudumishe Utamaduni wetu kwa Maendeleo ya Taifa".Hafla iliofanyika katika ukumbi wa Wizara hio Migombani Zanzibar.
Sabiha Khamis Maelezo
Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar limekusudia kurithisha mila, silka, desturi na maadili ya Mzanzibar kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo ili kuutambua na kuthamini Utamaduni wa Nchini yao.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar katika ukumbi wa Wizara hiyo Migombani amesema Tamasha hilo limekusudia kuikumbusha jamii kwamba Utamaduni wa Mzanzibar una vivutio vya aina yake ikiwemo burudani hivyo ni vyema kuuenzi na kuulinda.
Amesema utamaduni huo ni tunu na hazina kubwa ya Taifa ambao ni kivutio cha watalii wanaokuja nchini ambao ni chanzo kikuu cha pato la taifa.
Aidha amesema Tamasha hilo litaanzia Unguja na kumalizia Pemba lengo kuwarithisha vijana shughuli za kiasili pamoja na kuwaunganisha Wazanzibar jambo ambalo itasaidia kuleta maendeleo Nchini.
Amefahamisha kuwa katika Tamasha hilo wajasiriamali watapata fursa ya kuuza bidhaa zao ambazo zitasaidia kuitangaza nchi na kujipatia kipato kitakacho wasaidia kujikwamu kimaisha.
Amesema Tamasha hilo litajumuisha maonesho na shughuli mbali mbali ikiwemo maonesho ya bidhaa za kiutamaduni, wasanii wa fani tofauti, zana na vifaa vya utamaduni, dawa za asili pamoja na michezo mbalimbali hivyo ni vyema kuwaunga mkono wajasiriamali kwa kununua bidhaa hizo ili kuuendeleza utamaduni huo.
Ameeleza kuwa Wizara inajipanga kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga kituo cha ujasiriamali ambalo litakuwa na uwezo wa kuonesha kazi za kiutamaduni pamoja na makumbusho yatakayoonesha asili ya Mzanzibar ilipotokea mpaka ilipofikia.
Akitoa wito kwa wazazi na walezi kufika na watoto wao katika Tamasha hilo ili waweze kujionea utamaduni wa nchi yao pamoja na kujifunza asili ya Mzanzibar ilipoanzia.
Ufunguzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar litaanzia Unguja tarehe 19, Septemba 2024 katika uwanja wa Msuka, Mahonda mgeni rasmin anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kumalizika tarehe 22, Septemba 2024 kwa kuwafanyia Mahafali ya vijana waliojiendeleza katika Nyumba ya sanaa ambapo kauli mbiu ni "Tudumishe Utamaduni wetu kwa Maendeleo ya Taifa".
No comments:
Post a Comment