SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inakusudia kujenga kiwanja chengine kikubwa
cha kisasa chenye hadhi ya kimataifa, kitakachotumika kwenye michuano ya AFCON, mwaka 2027.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema
hayo alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa viwanja vipya vya michezo
Maisara (Maisara Sports Complex), Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi,
ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza Serikali imelenga kujenga
viwanja vya kisasa vya michezo kila wilaya pamoja na “Sprots Academy” kila
Mkoa.
“Tuna dhamira ya kweli ya kujenga uwanja wa kisasa
wa AFCON utakao fanana na ule wa “Old Traford” wa Manchester United ya Uingereza”
Alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.
Aidha, ameeleza Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania pamoja na Kenya na Uganda watakuwa wenyeji wa michuano ya AFCON
mwaka 2027.
Dk. Mwinyi amesema Serikali pia inakusudia kufanya marekebisho makubwa
ya viwanja vya Gombani Kisiwani Pemba na Uwanja wa Mao Tse Tung, Unguja lengo ni
kuwa na viwanja vya kisasda vyenye hadhi vitakavyokuwa chachu ya kuwainua
vijana kimichezo.
Ameongeza kuwa dhamira nyengine ya Serikali ni kujenga kiwanja cha mpira wa ufukweni (Beach soccer) kwa
hadhi ya kimataifa na kujenga bwawa kubwa la kuogelea (Swimming pool) lenye hadhi
ya Olympic, (Olympic size Swimming pool)
Amebainisha kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisononeshwa kwa kuwepo
viwanja vibovu vyenye vumbi na matope ambavyo vijana walivitumia kuchezea
michezo mbalimbali ikiwemo soka, alieleza hali hiyo imepitwa na wakati, hivyo serikali
imejiandaa kujenga viwanja vipya ili kutoa fursa kwa vijana kinua vipaji vyao
na ushindana kimataifa.
Ameeleza bado Zanzibar ina nia ya kurudi tena kuwa mwanachama wa
Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) hivyo ujenzi wa viwanja hivyo ni chachu
ya itakayoleta ushawishi wa kupata uanachama huo.
Amefahamisha kuwa
kuna kila sababu ya Zanzibar kuwa mwanachama wa CAF kwa sababu ina timu mahiti
ya “Zanzibar Herros” inayoweza kuleta ushindani na kuleta vikombe nchini.
Amesema, lengo ni
kuongeza vipaji ili Zanzibar iwe mshindani wa kimataifa katika nyanja mbalimbali
za michezo.
Akizungumzia uwanja
wa mpya wa Maisara (Maisra Sports Complex) aliouwekea jiwe la msingi, Rais Dk.
Mwinyi ameishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa kusimamia
ipasavyo, maendeleo ya ujenzi huo ambao kwa kiasi kikubwa utaimarisha sekta ya
michezo nchini.
Pia Dk. Mwinyi ameeleza
kuwepo kwa viwanja vya mpira wa kikapu (basketi ball), mpira wa wavu (volleyball),
mpira wa mikono (hand ball) na mchezo wa “Long tennis” kutatoa mazingira bora kwa
vijana kujifundisha michezo hiyo na kuzalisha vipaji zaidi.
Aidha, amefurahishwa kuwepo kwa kituo
cha mazoezi ya viungo kiwanjani hapo (fitness center) pamoja na viwanja vya
kufurahishia watoto (Children playground).
Akiizungumzia kaulimbiu ya miaka 61 ya
Mapinduzi ya Zanzibar isemayo “Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo yetu” aliwasihi wananchi kutokubali kufitinishwa ili
maendeleo zaidi yaendelee kupatikana katika sekta mbalimbali.
“Bila ya Amani, Umoja na Mshikamano hakuna
suala lolote la maendeleo litakalofaikiwa” alibainisha Rais Dk. Mwinyi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amesema wizara
itaendelea kutekeleza na kufuata maelekezo na miongozo inayotolewa na Rais Dr. Mwinyi
kwa kukamilisha miradi yote inayosimamiwa na Wizara hiyo kwa wakati na
mafanikio.
Ameeleza kuwa kinachofanyika hivi sasa
katika viwanja vya michezo Unguja na Pemba ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
ya CCM, 2020 -2025 kwa vitendo.
Waziri Tabia pia amemuhakikishia Rais Dk.
Mwinyi kutunzwa na kulindwa kwa viwanja vyote vinavyoojengwa ili viendelee
kutumia kwa miaka mingi iyajo.
Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo, Fatma Hamad Mbarouk, amesema ujenzi wa viwanja vipya vya “Maisara
Spots Complex” ulianza Septemba 2024 na unatarajiwa kukamilika kwake Machi 2025
ambapo kwasasa umefikia asilimi 60 ya ujenzi wake na mkandarasi anaendeleza
ujenzi huo kwa kasi inayoridhisha.
Amesema, Ujenzi wa viwanja vipya vya
michezo vya Maisara ni miongoni mwa ujenzi wa viwanja 17 vya michezo Unguja na
Pemba vyenye viwango vinavyokubalika na CAF na FIFA.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment