Habari za Punde

Bank of Africa Tanzania imejipanga kuwapatia huduma bora za kidigitali wateja wake Zanzibar

 

Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Hamid Seif Said akiongoza waalikwa katika iftar iliyoandaliwa na Bank of Africa Tanzania  kwa wateja wao iliyofanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar. 

Wananchi na wakazi wa Zanzibar wameaswa kuendelea kuchangamkia huduma na bidhaa kutoka Bank of Africa Tanzania kwa sababu serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatambua mchango wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza kwa uchumi wa wananchi.

Akizungumza kwenye Iftar iliyoandaliwa na benki hiyo mwishoni mwa wiki mjini Mtoni, Unguja, Zanzibar,  Mkurugenzi Mtendaji wa  Bank of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma aliwataka wazanzibari kuchangamkia fursa za huduma na bidhaa zinazotolewa na benki hiyo visiwani.

“wajasiriamali na wafanyabiashara wa Zanzibar wanaweza na waendelee kuitumia benki hii kwani ni rafiki kwa  wenye kipato cha kati, cha chini na kidogo kabisa.” alisema.

Amesema benki hiyo ina masharti nafuu na rahisi katika kumuwezesha mjasiriamali ili aweze kuyafikia malengo yake aliyojiwekea.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Hamid Seif Said amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Bank of Africa Tanzania unaochangia ukuaji wa uchumi watu wa Zanzibar na nchini  kwa ujumla.

Aliyasema hayo baada ya Iftari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake na watoto yatima, iliyofanyika Hotel Verde iliyopo Mtoni Unguja.

Hamid aliishauri uongozi wa benki  hiyo kuendelea kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo ya nchi ikiwemo upatikanaji wa miundombinu inayovutia kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Alieleza kuwa nchi nyingi zimeendelea ni kutokana na mchango wa wadau wa maendeleo na wawekezaji na kukiri kuwa  hata maendeleo ya Zanzibar yamekuwa yakiimarika  kutokana na mchango mkubwa kati ya serikali na sekta binafsi ikiwemo Bank of Africa Tanzania.

Alifahamisha kuwa Mapinduzi ya kiuchumi huanzia na mifumo ya kidigitali ambayo  inarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha  na kupunguza mwanya wa rushwa na kurahisisha upatikanaji wa mitaji kupitia taasisi za kifedha ikiwemo Bank of Africa Tanzania.

Aliwashukuru watendaji wa Benki hiyo kwa kuandaa Iftari hiyo ambayo ina akisi thamani na mchango wa wateja wao na wazanzibari kwa ujumla.

Kwa upande wake Meneja wa Bank of Africa Tanzania Tawi la  Zanzibar, Anas Ramadhan amesema vita ya maendeleo ya uchumi inahitaji mashirikiano kati ya wananchi na wawekezaji na kuwasisitiza  wananchi  kuiunga mkono benki hiyo kwa manufaa na maslahi ya pamoja.

Amesema benki hiyo  imewekeza Zanzibar na kuunga mkono shughuli za maendeleo na kuwa ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar (SMZ) kupitia mkakati wa uchumi wa Bluu.

Alieleza kuwa kitendo cha wateja wao kuwepo pamoja na watoto yatima na waumini wengine wa dini ya kiislamu katika Iftari hiyo ni heshima kwao kwani kinaonesha namna walivyojenga mahusiano ya muda mrefu na endelevu baina yao.

Amesema benki hiyo imewekeza katika njia tofauti za kidigital kama huduma za mawakala ambapo hadi sasa wana mawakala 20 na wanatarajia kuongeza hadi kufika 50 Ili kuwafikia watu wengi zaidi katika huduma zao.

Amesema hatua hiyo ni mkakati wa kuwafikia na kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi na kueleza kuwa  wanajivunia kuanzisha  mfumo wa Bnak of Africa Tanznaia malipo ambao inaifanya nchi kutumia  fedha zao kidigitali na kusaidia  kukusanya mapato kisasa.

Mbali na hayo amesema pia benki hiyo  imeanzisha huduma ya lipa namba ili kuisaidia Serikali katika kuondokana na matumizi ya  fedha taslimu ambayo yanachangia upotevu wa fedha.

Alifahamisha kuwa benki hiyo itaendelela kuwekeza katika huduma za kidigital na kuziboresha ili kuhakikisha nchi  inakwenda sambamba na  mabadiliko ya teknolojia.

Aliahidi kuendelea kushirikiana na kuunga mkono mipango ya Serikali ili kuhakikisha wateja wao wanachangia maendeleo ya kiuchumi.

Akitoa nasaha kwa waumini walioshiriki iftar hiyo, Sheikh Mohammed Ibrahim Khamis kutoka Masjid Maisara aliwataka waumini kuendeleza mema  waliyojifunza katika mwezi mtukufu wa Ramadhan hata baada ya kumalizika kwake.

Aidha aliwakumbusha kufanya ibada za usiku  kwa lengo la kuitafuta lailatul qadir hasa katika  kumi la mwisho la kumalizia mwezi huo.

Mbali na hayo aliwasisitiza kutoa sadaka na zakatul fitri sambamba na kusindikiza saumu zao kwa kutenda mema.

Meneja wa Bank of Africa Tanzania, Tawi la Zanzibar, Anas Ramadhan akizungumza katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Benki hiyo kwa wateja wao, iliyofanyika Mtoni, Unguja,  Zanzibar.
Wafanyakazi na Wateja wa Bank of Africa Tanzania wakiwa katika Iftar iliyoandaliwa na benki hiyo iliyofanyika Mtoni Unguja,  Zanzibar.
Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Hamid Seif Said akizungumza katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Bank of Africa Tanzania kwa wateja wake iliyofanyika Mtoni, Unguja  Zanziba

Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania , Esther Cecil Maruma akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Hamid Seif Said na Meneja wa Benki hiyo Zanzibar Anas Rmadhani wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Iftar iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake visiwani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.