Habari za Punde

Serikali Yapiga Marufuku Kutumia Misumeno ya Mnyororo Bila Kibali

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi akijibu maswali kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) leo tarehe 5 Mei, 2025 bungeni jijini Dodoma.

Serikali imepiga marufuku matumizi ya mashine aina ya msumeno mnyororo (chain saw) kukatia miti bila kibali kutoka mamlaka husika ili kupunguza kasi ya uharibifu wa uoto wa asili na mazingira kwa ujumla.

Sanjari na hilo pia imesema katika kukabiliana na janga la ukataji holela wa miti, hekta takribani millioni 5.2 za maeneo yaliyoharibiwa zinatarajiwa kupandwa miti ifikapo mwaka 2030.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi amesema hayo leo tarehe 5 Mei, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) lililoulizwa na Mbunge wa Moshi Vijijini Mhe. Prof. Patrick Alois Ndakidemi aliyetaka kujua tamko la Serikali kwa watu wanaovuna miti kwa kutumia misumeno mnyororo na hivyo kuwa kikwazo katika juhudi za kuhifadhi mazingira.

Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Katambi amesema kuwa pamoja na kwamba mashine hizo zinauzwa nchini upo utaratibu maalumu unaotoa mwongozo wa kufuata zisitumike ovyo kwenye maeneo ambayo hayajatolewa vibali.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais nitoe maelekezo ni marufuku kwa mtu yeyote kutumia chain saw bila kibali kutoka mamlaka zilizopo kwenye maeneo husika inayotambulika kisheria, kuna utaratibu wa namna ya kufanya uvunaji, tunaomba wazingatie hili kwani kwa ukiukaji wa taratibu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisisitiza.

Aidha, akijibu swali la msingi kuhusu upi mpango wa taifa wa kupanda miti kwa kipindi cha muda mfupi na mrefu ili kukabiliana na janga la kukata miti, Mhe. Katambi alibainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Maliasili na Utalii, inatekeleza mpango wa muda mrefu wa Mkakati wa Kurejesha kwa kupanda miti maeneo yaliyoharibiwa.

Naibu Waziri Katambi alisema katika mkakati huo miongoni mwa shughuli zinazoendelea ni pamoja na kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kupitia kampeni za upandaji miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa kila mwaka.

Alitaja mikakati mingine kuwa utekelezaji wa Kampeni maalumu ya Soma na Mti, ambapo Serikali inawataka wanafunzi wote wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kupanda miti na kuitunza katika kipindi chao chote cha masomo wawapo mashuleni na vyuoni.

Akiendelea kujibu swali hilo, alisema Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeendelea kuzalisha miche ya miti ya aina mbalimbali na kuigawa bure kwa wizara, taasisi, wadau na sekta binafsi ili waipande katika maeneo yao kurejesha uoto wa asili nchini.

Hivyo, ametoa rai kwa wananchi na sekta binafsi kuendelea kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na uharibifu wa ardhi na kuenea kwa jangwa na ukame.

Kwa upande mwingine amesema inagawa mazingira si suala la Muungano, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia viongozi wake inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia na kuweka mikakati kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu.

Naibu Waziri Katambi alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Khalifa Mohammed Issa aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kusimamia programu za upandaji wa mikoko na kuilinda ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.