Habari za Punde

BALOZI SEIF KUMUWAKILISHA DK SHEIN 'MAY DAY'

Asya Hassan na Kauthar Abdalla

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kumuwakilisha rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kilele cha siku ya wafanyakazi duniani ‘May Day’.

Katibu Mkuu wa shirikisho la Wafanyakazi Zanzibar, Khamis Mwinyi Mohammed alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Kikwajuni mjini hapa.

Kilele cha siku ya Wafanyakazi duniani hapo awali kilikuwa kifanyike katika kiwanja cha Amaan mjini hapa lakini habari zilizokuwepo ni kwamba sherehe hizo zitafanyika katika viwanja vya hoteli ya Bwawani, huku maandamano yakitarajiwa kuanzia viwanja vya Malindi.

Katibu huyo alisema kutokana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mainduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kuwa ziarani nchini Uturuki, Balozi Seif atamuwakilisha Rais kwenye hafla hiyo inayofanyika kila mwaka duniani kote.

Alisema siku moja kabla ya Rais kuondoka nchini, maofisa wa shirikisho hilo walipata fursa ya kuzungumza naye ambapo katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliwaomba radhi kutokana na kutokuwepo kwake kwenye sherehe hizo.

“Rais alituomba radhi nasi tumemuelewa kwani ziara yake ni muhimu kwa nchi yetu, na akatueleza kama ingewezekana zinge sogezwa mbele sherehe hizo, jambo ambalo haliwezekani”, alisema katibu huyo.

Katika hatua nyengine katibu huyo alisema ipo tamaa kubwa ya serikali kuwapandishia mishahara watumishi wake.

Alisema Rais ameahidi kuipandisha mishahara ya watumishi kauli ambapo pia imetolewa na baadhi ya mawaziri wanaohusika na masuala ya fedha na utumishi.

Hata hivyo katibu huyo alisema hajajua mshahara huo utapandishwa kwa kima gani kutoka kima cha chini cha shilingi 100,000 kwa mwezi hivi sasa.

Katibu huyo alisikitishwa na hali inavyoendelea ya wafanyakazi kuendelea kupokea mshahara usio na nyongeza kwa hata miaka 20.

“Mfanyakazi Zanzibar anaweza kupokeza kima cha chini kwa miaka 20 kama haijatokea fursa ya kupandisha mishahara”, alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.