Habari za Punde

JESHI LA POLISI LAWAMANI PEMBA

Ladaiwa kuziviigisha kesi za ubakaji, udhalilishaji

Mwalimu, Mganga, Polisi wadaiwa kutorosha, kubaka

Na Abdi Suleiman, Pemba

MRATIBU wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar tawi la Pemba, Azizi Hemed Mtela, amelitaka jeshi la Polisi kisiwani humo, kujisafisha kwa kufanyakazi kwa mujibu wa taratibu na kufuata sheria.

Alisema muda umefika kwa jeshi hilo kujisafisha na lazima tatizo la kesi za ubakaji wa watoto lipatiwe ufumbuzi wa kina kwa kufikishwa mahakamani watuhumiwa wa udhalilishaji.

Mratibu huyo alieleza hayo huko ofisini kwake Chake-Chake, alipokuwa akizungumza na gazeti hili, ambapo alifahamisha kuwa utendaji wa baadhi ya watumishi wa jeshi hilo unatia mashaka hali inayochangia matukio ya udhalilishai kutishia amani.

Azizi alisema kuwa jamii kwa kiasi kikubwa inaliamini jeshi la Polisi, ni wajibu wa jeshi hilo kushirikiana kwa dhati na wananchi ili kuweza kuwafichua wahalifu wa makosa mbali mbli wanayoyafanya ikiwemo udhalilishaji wa watoto.

Mratibu huyo alisema katika kipindi cha mwezi huu wa Aprili kituo chake kimepokea kesi kadhaa za ubakaji wa watoto, ikiwemo ya msaidizi mwalimu mkuu skuli ya Tumbe, Shehe Bakari Mwinyi, anayesadikiwa kumpa ujauzito mototo wa darasa la nne (4) mwenye umri wa miaka 13.

Aidha mbali ya tukio hilo, tukio jengine ni lile la mganga wa kienyeji Makame Abdalla Salim wa Kisiwa Panza, anatuhumiwa kumpa ujauzito binti katika mazingira ya kutatanisha, kwa madai njia ya kumwingilia ndio pekee ya tiba kwa ajili ya maradhi ya wasi wasi yaliyokuwa yakimsumbua binti huyo.

Aidha tukio jengine la udhalilishaji ni kwa askari polisi wawili wa kituo cha Kengeja, waliotambulika kwa jina moja moja tu, Khamis na mwenzake Juhudi, wanaodaiwa kuwatorosha mabinti wawili na baadae kuwabaka.

“Nasikitishwa sana kuona mtu aliyeaminiwa na serekali kwa ajili ya kuwasomesha watoto kama mwalimu halafu kusikia anampa ujauzito mwanafunzi wake tena wa darasa la nne, hii inaonesha dhahiri kuwa hajui wajibu wake, na kumuharibia maisha yake binti kama huyo je, yeye kama binti yake ataridhika”, alisema.

Alisema dada wa binti huyo alifika katika kituo cha Polisi Konde, Aprili 7 mwaka huu na kuambiwa arudi tena Aprili 11 mwezu huu, siku hiyo jioni yake alimkuta askari polisi Hamad Mwinyi Haji na Naibu sheha Seif Omar wakiwa pamoja na mtuhumiwa Shehe Bakari Mwinyi wamekaa pamoja, ambapo Aprili 12 dada huyo alipata taarifa kuwa mtuhumiwa ametoroka.

“Inasikitisha sana kwa vitendo vya baadhi ya askari polisi kutokuwa makini ‘serious’ na matukio kama haya mfano dada wa binti alienda kuliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi Konde lakini askari waliyekuwepo kituoni hapo wawakuwa makini na tukio hilo”,alisema Azizi.

Aidha alifahamisha kuwa mifano ya matukio hayo ni dhahiri kwamba yameeleweka kisheria kwamba ni makosa ya ubakaji, mganga kwa kutumia nafasi yake kutenda kosa hilo alilotenda ni wazi kwamba ni ubakaji chini ya kifungu cha 125 cha kanuni ya adhabu ya sheria namba sita 6 ya mwaka 2004.

Alifafanua kuwa halkadhalika kwa Mwalimu mkuu msaidizi huyo kwa kitendo cha kutumia wadhifa wake na kufanya hivyo alivyofanya ni ubakaji chini ya kifungu cha 125 kifungu cha kwanza sheria namba sita 6 mwaka 2004 ni ubakaji.

“Nashangaa kusikia mtuhumiwa ametoroka kwa sababu ametoka nje ya Pemba, ndio iwe ni basi na suali lile limekufa na mahakama isiendelee na shauri lile”,alisema Azizi.

Alisema kitendo hicho ni kitu ambacho jeshi la polisi linatakiwa kukiangalia kwa makini na kwa mapana yake ili kuweza kukomesha vitendo vya namna hiyo vya ubakaji wa watoto wadongo kwani ni kuwaharibia mustakbali wa maisha yao ya baadae.

Hata hivyo Azizi aliitaka jamii isivunjike moyo na iendelee kupeleka makosa yao katika kituo hicho cha sheria kiko mstari wa mbele wakishirikiana na jeshi la polisi katika kuhakikisha polisi wachache wanaotaka kulipaka matope jeshi hilo wanachukuliwa hatua kali na hatimaye haki inapatikana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.