Habari za Punde

BARCELONA KURUDIA YA 2009 LEO?

Inaivaa Manchester United Wembley katika fainali UEFA

Macho ya mashabiki yaelekezwa kwa Messi, Rooney

LONDON

MIAMBA ya soka barani Ulaya, Manchester United ya England na Barcelona ya Hispania, inashuka dimbani leo katika mchezo wa fainali kuamua kinara wa Ligi ya Mabingwa barani humo mwaka 2011/12.

Pambano hilo litakalochezwa katika dimba la Wembley mjini London, limekuwa gumzo kubwa kwa muda sasa tangu miamba hiyo ilipokata tiketi za kuwania taji hilo lenye hadhi kubwa barani Ulaya.

Kutokana na kila timu kupania kushinda na kunyakua taji hilo, hapana shaka mchezo huyo leo utakuwa wa ushindani mkubwa ambapo mamilioni ya wapenda soka duniani kote watakuwa wakiufuatilia kupitia katika televisheni, mbali na wale watakaopata bahati kutinga kwenye uwanja wa Wembley kushuhudia kimbembe hicho ‘live’.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu kwa wanaume hao kukutana katika fainali ya michuano hiyo, mara ya mwisho ikiwa mwaka 2009 mjini Rome, Italia ambapo Barcelona iliwatandika mashetani wekundu mabao 2-0 na kubeba ‘ndoo’.

Aidha kabla ya mchezo wa leo, timu hizo zimewahi kukutana mara 11 katika michuano hiyo, huku kila moja ikiibuka na ushindi mara tatu.

Sambamba na rikodi hiyo, kila moja kati ya timu hizo, imeshalitwaa kombe la mashindano hayo mara tatu.

Timu zote mbili zinateremka dimbani zikihamasishwa na mafanikio ya kushinda ubingwa wa ligi za nchi zao kwa msimu uliomalizika hivi karibuni, huku Manchester United ikiwa imetwaa ubingwa wa ligi hiyo mara nne katika kipindi cha miaka mitano na Barcelona imetwaa taji lake la tano katika kipindi cha miaka saba.

Ingawa vikosi vyote vinaundwa na wanandinga mahiri na nyota, lakini mashabiki wengi wa soka duniani watakuwa wakiwakodolea macho wachezaji wawili, Wayne Rooney wa Manchester United na Lionel Messi wa Barcelona.

Akizungumzia mtanange huo, Messi alikaririwa hivi karibuni, akisema kufunga magoli katika nyavu za Manchester United si kitu anachokilenga, bali muhimu kwake ni kuona timu yake inatwaa ubingwa huo ndani ya ardhi ya Uingereza.

Muargentina huyo anayefananishwa sana na nyota wa zamani wa nchi yake Diego Maradona, alisema hawapaswi kuidharau Manchester United kwa kigezo cha kuifunga katika mechi yao ya mwisho mwaka juzi, kwani kila mchezo unakuwa na mazingira yake.

“Siingii uwanjani kuwania ufungaji bora, kwangu mimi kitu muhimu na kitakachonipa raha ni kuona Barcelona inashinda taji kwa mara nyengine, kuliko kupachika magoli kwani sitakuwa peke yangu uwanjani”, alisema Messi.

Katika msimu huu, Messi ameipachikia Barcelona mabao 52, ambapo 11 ameyafunga katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya na kama atacheka na nyavu leo, anaweza kuifikia au kuivunja rikodi inayoshikiliwa na Ruud van Nistelrooy ya kufunga mabao 12 kwenye michuano hiyo.

Kwa upande wake, Wayne Rooney anaamini kuwa, baada ya kuisaidia Manchester United kutwaa taji la 19 la ligi kuu ya England, zawadi pekee iliyobaki kwa mashabiki wao, ni kuiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa Ulaya kwa mara ya nne.

Mshambuliaji huyo ghali nchini England kwa sasa, ambaye alichezea michuano ya fainali za Ulaya kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na kufunga mabao manne, amekuwa dhahabu kwa kikosi cha Sir Alex Ferguson na ameshinda tuzo ya mwanasoka bora wa England mara mbili mwaka 2008 na 2009.

Kufikia Machi mwaka huu, aliweka rikodi ya kucheza mechi 79 za kimataifa na kufunga mabao 26.

“Furaha yangu itatimia kama tutashinda leo. Katika soka kuna mambo mengi lakini haitapendeza kuona Barcelona inatushinda hata katika ardhi ya nchini kwetu”, aliiambia tovuti ya klabu yake.

Kwa vyovyote vile, makocha wa timu hizo, Pep Guardiola wa Barcelona na Alex Ferguson wa United, hawatarajiwi kutulia katika viti vyao, kwani ushindi kwao ndio utakaokuwa ukiwindwa na wote hao kwa udi na uvumba. (BBCFOOTBALL).


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.