Habari za Punde

KINU NA MCHI

Na Suleiman Almas

VIFAA vyenye asili moja katika kuundwa kwake tokea enzi na enzi si chini ya miaka mia moja nyuma. Ndoa hiyo imedumu kwa muda mrefu na kuendelea hivyo hivyo kwa kila kimoja kumtegemea mwenziwe katika utendaji kazi.

Kinu na mwenziwe mchi ni zana zilizotokana na maarifa ya kiafrika ambayo yamewawezesha waliotangulia kusaga aina kadhaa za nafaka na kuzisarifu wanavyotaka.

Ubunifu huo pia umechangia kujenga afya na misuli ya wahenga kutokana na matumizi yake yaliyowajumuisha kina mama na kina baba vijana hadi wazee wa wakati huo.

Kutwanga mpunga, mtama, mahindi muhugo kwa zama hizo hakukutumika mashine bali shughuli hiyo ilifanyika kupitia nguvu za mwili ikiwemo viungo vyote kufanya kazi kwa mashirikiano.

Hapo kabla zana hizo zilitengenezwa sambamba kwa maana ya fundi huyo huyo ni wa kinu na huyo huyo wa mchi tafauti na zama za leo vitu hivyo hununuliwa mbalimbali huku kasi ya matumizi ya vitu hivyo asilia ikipungua sawa na utengenezaji wake kuonekana kushuka kutokana na sababu lukuki.

Sababu kuu ya kwanza ni ile kushuka kwa idadi ya wataalamu wa uchongaji na jamii kuelekea sana katika mashine, Mazingira ya miji nayo hukataza kinadharia kutumika kwa zana hizo zilizo na uhakika wa kukoboa kwa wakati anaojipangia muhitaji.

Inapozungumzwa watu wa zamani walikuwa wakiishi muda mrefu hali hiyo ilitokana na mambo mengi ikiwemo na kazi walizokuwa wakizifanya kwa tafsiri ya kujituma na vyakula walivyotumia wakati huo.

Kimtizamo wa haraka haraka kuzungumzia suala kama hilo la kinu na mchi, inawezekana kabisa kufikiria kuwa hakuna haja ya kurudi nyuma kwenye enzi za vitu hivyo, ingawa historia na asili haiwezi kupotea moja kwa moja baadhi huthubutu kusema hujirejea.

Iwapo vijana wakifunzwa kuzitumia zana za kiasili bila shaka watafundishwa na kuzitengeneza, ni moja katika faida ya kujitafutia ajira kupitia raslimali ziliopo ndani ya nchi.

Vitu mchi na kinu kwa sasa kuonekana na kutumika kwake pengine ni vijijini, kwa baadhi ya maeneo bado wanaendelea na utamaduni wa kutwanga na kuchunga hususan baada ya mavuno.

Kazi hiyo hakika ni ya Kiafrika inaamanisha ni sehemu ya ukakamavu ambao ilitakiwa kurithiwa kutoka kizazi hadi kizazi chengine badala kujivunia uvivu.

Msisitizo wa matumizi wa mambo ya kiasili utabaki palepale mijini na vijijini ili kuondokana na tamaduni za mapokezi ambazo kwa makusudi huingizwa kudumaza maarifa ya kiasili yaliyotumika na wahenga.

Ukweli uliowazi mtama wa kutwanga kwa kinu unakuwa tafauti kubwa na wa kusagiisha kwa mashine ambapo kuna baadhi ya vitu hukosekana baada ya matayarisho ya upatikanaji wa unga.Kinu unaweza kukosha na kutumia kutwangia vitu tafauti lakini mashine inakuwa ni vigumu kufanyika kwa hayo.

Kuishajiisha jamii kuthamini zana za kiasili si jambo gumu wala baya kwa kuwa ni taaluma inayotokana na Mali asili ziliopo ndani ya nchi haihitaji kuagizwa kutoka Mataifa ya ng'ambo.

Vijana wanayo nafasi kubwa ya kujiajiri kwa kutumia vyombo vya kiasili wawe wanawake au wanaume kwa kila mmoja na fani inayomuhusu kutokana na uasili wake wa utengenezaji kutoka kwa waasisi.

Kwa mfano ufinyazi wa vyungu na mikungu, ususi na mapishi ya kiasili kinadada wanaweza kujikita katika maeneo hayo huku akina kaka wakajituma katika fani za uundaji kupitia kuchonga vitu mbalimbali vinavyotokana na raslimali miti.

Maslahi ya zana hizo ni makubwa katika majra yaliopo, kinu kwa sasa hakipungui shilingi 10,000 kikiwa ni pekee, mbali mwenziwe mchi na kama ijulikanavyo bila ya mchi kinu hakina maneno na bila ya kinu mchi hauna pakwenda.

Jamii ni vizuri ikatumia fursa ya matumizi ya nyenzo asilia kuendeleza utamaduni wa kuthamini ufundi na maarifa ya wazee waliopita wakati huohuo kutumia zana za kisasa kwa yale yaliyokuwa hayakuwahi kubuniwa na wahenga.

Njia nyengine inayofaa, pamoja na kwenda na wakati kiteknologia si jambo muafaka kusahau uasilia kwa vile bado ipo faida kwa jamii inayoishi sasa na ile inayokuja

1 comment:

  1. Hilo neno kinu na mchi lina tafrisi nyingi na sisi wazanzibar ni walimu wa kuitumia lugha ya kiswahili kufikisha ujumbe tutakao ,Lol hatari lakini salama


    Taufiq bin Takadiri

    wa Mchamba wima

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.