Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amewaongoza maelfu ya wananchi na viongozi mbali mbali wa kitaifa, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya Mashujaa.
Maadhimisho hayo yamefanyika jana katika viwanja vya Naliendele Mjini Mtwara eneo ambalo pana makaburi ya mashujaa waliopigana vita vya Msumbiji.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Waziri wa Ulinzi na Majeshi ya Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Philipe Nyasi.
Wengine ni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Ramadhan Haji, baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Wakuu wa vikosi vya Ulinzi wa Tanzania na Msumbiji, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania, Majenerali wastaafu waliopigana vita vya Msumbiji pamoja na vita vya dunia na viongozi wengineo.
Katika maadhimisho hayo kama ilivyo kawaida baadhi ya viongozi akiwemo Rais Kikwete waliweka silaha za asili ambapo kwa uande wake aliweka Mkuki na Ngao, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange aliweka sime, Kiongozi wa Mabalozi, Balozi wa DRC, Balozi Juma Khalfan aliweka shada la maua ambapo Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mstahiki Suleiman Mtalika aliweka upinde na mshale.
Baada ya tukio hilo dua na sala kutoka kwa viongozi wa Dini zilizomwa ambapo Sheikh Jamaldin alisoma dua kwa upande wa Waislamu, Mchungaji Lucas Mendule aliwakilisha Kanisa la CCT na Kanisa Katoliki liliwakilishwa na Padri Gabriel Mule.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na baadhi ya viongozi wengine wakuu walitembelea makaburi ya mashujaa hao na baadae kuwasalimia wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, ambapo katika salamu zake Rais Kikwete alieleza kuwa kila mwaka Taifa limekuwa na utaratibu wa kuhifadhi kumbukumbu za mashujaa na kutoa pongezi kwa wananchi wengi kujitokeza katika maadhimisho hayo.
Rais Kikwete alisema kuwa kabla ya sherehe hizo kufanywa tarehe hiyo ya jana hapo mwanzo zilikuwa zikifanyika Septemba mosi kutokana na kumbukumbu za kuwapokea Majeshi kwa ushindi walioupata huko nchini Uganda.
Alisema kuwa hivi sasa kila ifikipo tarehe 25 husherehekea maisha ya wakombozi hao kutokana na juhudi kubwa walizozifanya katika kuikomboa nchi ya Msumbiji na sio kusherehekea kufa kwao.
Akieleza historia ya mashujaa hao kwa ufupi, Rais Kikwete alisema kuwa wanajeshi wa Tanzania waliokufa nchini Masumbiji katika jitihada za kuikomboa nchi hiyo kutoka kwa Wakoloni wa Kireno.
Alieleza kuwa Tanzania ilitoa msaada mkubwa katika vita hivyo kutokana na kiongozi wa FRELIMO wakati huo hayati Samora Mashel kumuomba hayati Mwalimu Nyerere kusaidiwa mafunzo na hatimae Majeshi ambapo pia, baada ya ukombozi huo kulitokea watu wachache waliokuwa hawakufurahishwa na ukombozi huo na ndipo walipowatumia waasi wa RENAMO na kuanzisha vita vingine.
Alieleza kuwa katika mapambano ambapo hatimae walisambaratishwa na Majeshi ya Msumbiji kwa mashirikiano na Majeshi ya Tanzania na ndipo baadhi ya wanajeshi wa Tanzania walipoteza maisha katika vita hivyo.
Aidha, alieleza kuwa Mashujaa hao awali walizikwa nchini Msumbiji na baadae ndipo ikaamuliwa kuzikwa katika eneo hilo ambapo pia, alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa Jeshi la Tanzania kwa kuwawekea mazingira mazuri mashujaa hao.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapainduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa wananchi wa Mtwara kwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kuwapa salamu za wananchi wa Zanzibar.
Nae Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji alieleza kuwa uhuru wa Msumbiji ulitokana na damu za Mashujaa hao na kupelekea nchini yao hivi sasa kuendelea kuwa na amani na utulivu mkubwa.
Baada ya hapo viongozi hao wakuu kwa pamoja pamoja na viongozi wengine wakiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete walitembelea nyumba ya Makumbusho ya Naliendele iliyopo katika eneo hilo ambapo mna vifaa mbali mbali vilivyotumiwa na mashujaa hao katika ukumbozi wa Msumbiji. Katika maadhimisho hayo mizinga ilipigwa pamoja na wimbo wa Taifa sambamba na kutolewa salamu za Rais.
No comments:
Post a Comment