Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kutoa msaada wa hali na mali kwa ajili ya kuziwezesha Asasi za kiraia zitazotoa elimu ya uraia kuhusu katiba na kuhamasisha jamii kujitokeza katika mchakato wa zoezi zima la upatikanaji wa katiba mpya.
Wito huo umetolewa leo na Mjumbe wa Baraza la Katiba Zanzibar ambaye pia ni Mwanasheria wa kujitegemea Awadh Ali Said huko katika ukumbi wa Zanlink Majestic alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maoni ya Baraza hilo juu ya Sheria ya mabadiliko ya katiba No. 8 ya mwaka 2011
Amesema kama Serikali itakuwa tayari juu ya jambo hilo Asasi hizo zitatekeleza jukumu la kuwahamasisha wananchi ili waweze kufanya maammuzi sahihi katika kutoa maoni yao juu ya mchakato wa katiba mpya.
Mwanasheria huyo amesema jamii inapaswa ishirikishwe kwa upana wake katika mchakato wa Katiba ili ukubalike na kuridhiwa na wananchi jambo litakalowapelekea wasijione wametengwa katika maandalizi ya mchakato huo
Amesema ni muhimu pia kuwepo kwa mjadala wa kitaifa juu ya sheria hiyo ili kujenga mwafaka wa kitaifa katika jambo lililo muhimu katika uhai wa taifa.
Kuhusu muundo wa tume Awadh alisema uteuzi wa Wajumbe wa Tume hiyo ni vyema wajumbe wake wapate ridhaa ya Baraza la Wawakilishi au Bunge la Jamhuri ya Muungano vyombo ambavyo ni viwakilishi halali vya wananchi na hivyo kuondoa hofu kuwa tume hiyo imetawaliwa na kiongozi fulani
Aidha amependekeza wajumbe wa tume waendelee kubaki katika Bunge maalum hata baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge hilo ili waweze kutimiza wajibu wa kutoa ufafanuzi pale itakapostahiki.
Akielezea kuhusu kipengele cha Muungano Mwanasheria huyo alieleza kuwa kifungu cha 9(2) cha hadidu za rejea hakiweki wazi majadala wa Muungano na hivyo kupendekeza kuwepo uwazi juu ya mjadala wa Muungano
Aidha Mwanasheria huyo alipendekeza Bunge Maalum la Katiba kutokuwa na utashi wa kisiasa wa kivyama na badala yake wajumbe wa baraza hilo wajali maslahi ya taifa na siyo itikadi za vyama vyao katika kupata katiba mpya.
No comments:
Post a Comment