SHEHA wa Shehia ya Paje, Ramadhan Mohammed Ahmada amesema kuna maharibiko makubwa ya kitabia kwa vijana wa kijiji hicho ambapo hivi sasa biashara ya dawa za kulevya imekuwa kama biashara nyengine za kawaida.
Sheha huyo alieleza hayo kwenye mahojiano maalum na gazeti hili, huko Paje wilaya ya Kusini Unguja, ambapo alisema vijana wamebadilisha maadili mazuri waliyokuwa nayo watu wa Paje.
Alisema biashara ya mihadarati imekuwa ya kawaida na wanaouza wanajulikana, hali ambayo imekuwa ikichangia kuibuka kwa vitendo viovu na vichafu kila uchao.
“Hivi sasa Paje imeharibika tofauti na ile iliyokuwa ikifahamika, unga unauzwa kama kawaida na wauzaji wanajulikana wapo hapa hapa mitaani”, alisema Sheha huyo.
Aidha alisema dawa za kulevya zimeporomosha uchumi wa vijana kwani hawendi baharini kuvua, huku mchana kutwa wakisinzia pamoja na kupita wakizurura.
Alisema mbali ya unga pia wapo maajenti maalum wanaosambaza biashara ya bangi ambayo nayo imekuwa ikitumiwa na baadhi ya vijana wenye umri kati ya miaka 16 hadi 30 kutoka kijiji hicho.
Alishangazwa na tabia ya watu hao wanaotuhumiwa kuuza unga na bangi kukamatwa na baada ya muda mfupi huonekana wakidunda tena mitaani, huku akishuku kuwepo mazingira ya rushwa.
Sheha huyo alivitaja vitendo vinavyochangiwa na biashara ya dawa za kulevya ni pamoja na kuibuka kwa ukahaba ambao unafanywa na wageni kutoka nje ya kijiji hicho.
“Haya Paje kuwa na makahaba ni mapya, lakini ndio tunayona hivi sasa wageni wamekodi nyumba na kutoa huduma zao”,alisema Sheha huyo.
Aidha alisema hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la wizi wa vitu mbali mbali ikiwemo mifugo ambayo imekuwa ikiibiwa na kuchinjwa halafu watu kuuziwa nyama.
Akizungumzi kupigwa mziki wakati wa usiku, alisema kwa kiasi jambo hilo limewezekana huku ikibakia sehemu moja tu ambayo imekuwa ikikaidia amri ya kutopiga mziki kwa sauti kubwa wakati wa usiku.

WATANGANYIKA WAFUKUZENI JAMAANI
ReplyDelete