Habari za Punde

Skuli Zatakiwa Kuhifadhi Mazingira

Na Masanja Mabula – Pemba

Afisa Tawala Wilaya ya Micheweni, Ahmed Halid, amewataka walimu na wanafunzi katika wilaya hiyo kuziimarisha klabu za mazingira katika skuli zao ili zitumike katika kuyahifadhi, kuyalinda na kuyatunza mazingira yanayowazunguka .

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Utumishi Wilaya hiyo, Mbwana Hamad, katika shamra shamra wa maadhimisho ya siku ya Maziingira Duniani katika Viwanja vya Polisi Konde, alisema kuimarishwa kwa klabu hizo kutaleta ufanisi wa uhifadhi wa mazingira .

Alisema baadhi ya Skuli zinaonekana kushindwa kuziimarisha klabu za mazingira katika skuli zao jambo ambalo linawafanya wanafunzi kushindwa kutambua umuhimu wa mazingira katika maendeleo na ustawi wa binadamu.

“Klabu za mazingira zinasaidia sana kuwajenga wanafunzi kujua umuhimu wa mazingira pamoja na athari zinazoweza kupatikana endapo jamii itashindwa kuyatunza, hivyo nawasihi muziimarishe ili ziweze kutumika katika utoaji wa elimuya mazingira kwa wananchi," alifahamisha .

Naye, Afisa wa Mazingira Wilaya ya Micheweni, Salum Mjaka, akizungumza na Zanzibar Leo, alisema bado elimu ya mazingira inahitaji kutolewa kwa wananchi wa Wilaya hiyo ili waachane na vitendo vya uchimbaji wa mchanga, mawe na matofali .

Alisema vitendo hivyo mbali na kuchangia uharibifu wa mazingira bali pia vimesababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha yao kwa kuangukiwa na mawe wakati wakiwa katika shughuli za uchimbaji na uokotaji wa kokoto.

Aidha alisema juhudi za makusudi zinahitaji kuchukuliwa na jamii yote katika kusimamia suala la uhifadhi wa mazingira kwa kujiepusha na vitendo vinavyopelekea kuwepo na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti ya aina mbali mbali katika maeneo ya machimbo ya mawe na mchanga.

“Suala la utunzaji wa mazingira linahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya asasi , jamii na mashirika na tuondokane na mtizamo hasi ya kwamba suala hili ni kazi ya Idara ya Mazingira na taasisi teule , bali kila ashiriki kwa mujibu wa nafasi aliyonayo," alisema.

Katika shamra shamra hizo ambazo ziliwajumuisha wanafuzi kutoka Skuli ya Wingwi, Msuka, Konde na Kinowe mbali na kufanyika usafi wa mazingira pia zilitumika kwa mechi ya mpira wa miguu kati wa wanafunzi wa Skuli ya Wingwi na Msuka .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.