Habari za Punde

Balozi Seif: Jitokezeni kuhesabiwa

Na Mwashamba Juma
MAKAMO wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi amesema zoezi la sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012, ni muhimu na hailengi kutafuta dini ya mtu bali ni kutafuta idadi ya Watanzania ili nchi iweze kupanga maendeleo.

Balozi Seif alieleza hayo jana huko katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Zanzibar Tunguu, wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku 12 kwa ngazi ya mkoa kwa wakufunzi wa sensa ya watu na makaazi inayotarajiwa kufanyika nchini kote mwezi ujao.

Alisema kwa upande wa Zanzibar, lengo la sensa ni kuitambua idadi halisi ya wakaazi wa Zanzibar, hali itakayosaidia kuharakisha uandaaji wa sera na utekelezji wa dira na mipango ya maendeleo.

Alisema zoezi la kuhesabu watu litaanza Agosti 26 mwaka huu, na kuendelea kwa siku saba ambapo kila mtu atakaelala nchini atahesabiwa, hivyo aliwataka wananchi kutunza kumbukumbu za taarifa kwaajili ya mauali yatakayoulizwa na makarani wa sensa.

Alifahamisha kuwa taarifa za matokeo ya takwimu zitakazokusanywa zitabakia kuwa ni siri kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2007 ya ofisi ya Mtakwim Mkuu Zanzibar, pamoja na sheria ya takwim ya mwaka 2002 ya ofisi ya Taifa ya takwimu.

Balozi Seif alisema kazi ya kuhesabu watu haitiathiri shughuli za uchumi au jamii kwani makarani wa sensa watapita katika kila kaya na kila mtu atakaelala nchini usiku wa sensa atahesabiwa mara moja na si zaidi ya hapo.

Aliwataka wakufunzi hao kuwa makini katika mafunzo hayo na kuwa tayari kupokea kile watakachowasilishiwa kwao

Alisema uingizwaji wa takwimu za sensa kwenye komputa utafanikiwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa kama iliyotumika katika sensa ya mwaka 2001, teknolojia ambayo ilipata mafanikio makubwa ya kutoa matokeo ya awali ndani ya miezi mitatu mara baada ya kuhesabiwa watu.

Alisema mafanikio ya teknolojia hiyo yaliipatia heshima kubwa nchi katika nyanja za kimataifa na kupelekea baadhi ya nchi za Afrika kujifunza kutoka kwetu, miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na Ghana, Ethiopia, Eritrea, Angola, Sudan, na Lethostho.

Aliwataka wabunge, wawakilishi, madiwani, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, masheha na watendaji wengine kushirikiana kwa pamoaja katika kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusiana na sensa.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa serikali, Mohammed Hafidh Rajab alisema kuwa kuwa changamoto kubwa inayoikabili sensa ya mwaka huu ni kuhusiana na masuala ya dini ambapo inaelekea kuathiri mitazamo ya wengi.

Mtakwimu huyo aliwaomba Wazanzibari na waumini wa madhehebu yote kutowa ushirikiano katika kuwafikishia wananchi umuhimu wa sensa kwaajili ya maendeleo ya taifa.

Mohammed alisema sensa itaangalia zaidi masuala ya idadi ya watu, hali zao, uchumi, jamii ikiwemo aina mbalimbali za maradhi ili serikali iweze kujipanga na ujenzi wa huduma za jamii kama vituo vya afya, skuli na maji safi.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 idadi ya wakaazi wa Zanzibar ilifika 940,000 ambapo kwa mwaka huu inakadiriwa jumla ya Wazanzibari 1.2 milioni.

Aidha mafunzo hayo yaliwashirikisha maofisa mbalimbali wa kutoka wizara ya Elimu na waratibu elimu na kutakiwa kutumia taaluma zao kwa umakini mkubwa na kuhakikishia kuwa watafanya kazi kwa uweledi na ufanisi mkubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.