Miembeni yakubali kuiachia kiti
Makungu asema nia ni kumaliza migogoro
Na Salum Vuai, Maelezo
KLABU ya soka ya Miembeni SC, imejitoa muhanga na kusamehe nafasi yake ya kucheza ligi kuu ya Zanzibar msimu ujao, na kuipisha timu ya Malindi, iliyokuwa ikisisitiza Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kitekeleze amri ya mahakama kutaka irejeshwe baada ya awali kuteremshwa madaraja mawili.
Kwa mujibu wa barua ya ZFA Taifa iliyoandikwa Julai 27, 2012 kwenda kwa uongozi wa Malindi yenye nambari ya kumbukumbu ZFA/MAL/VOL. 7/202, Malindi imetakiwa ijiandae kwa kufuata taratibu zote za matayarisho yanayostahili kwa mujibu wa kanuni ili iweze kucheza ligi kuu msimu ujao.
ZFA imesema hatua hiyo imekuja baada ya mashauriano kati ya Miembeni na kamati tendaji ya chama hicho, kwa nia ya kujenga mustakbali mzuri wa soka la Zanzibar.
Aidha, kutokana na uamuzi huo, Miembeni SC imekubali kucheza daraja la kwanza kanda, kujaza nafasi ya Mundu ambayo ilishuka kutoka ligi kuu msimu uliomalizika.
Akizungumzia uamuzi huo, Rais wa ZFA Amani Ibrahim Makungu, amesema hatua hiyo imelenga kumaliza migogoro ndani ya chama hicho, kwa manufaa ya soka la Zanzibar na kuendelea kupata imani ya wadhamini.
Alifahamisha kuwa, bila kuchukua uamuzi huo, huenda ligi kuu na hali nzima ya hewa katika soka la Zanzibar ingeendelea kuishi katika mivutano, kwani Malindi ilikuwa imepania kudai haki ya kucheza ligi kuu, iking'ang'ania amri ya mahakama itekelezwe.
"Mimi niliahidi kumaliza migogoro katika ZFA ili kumfariji Mheshmiwa Rais Dk. Shein ambaye alieleza wazi kuchoshwa na hali hiyo, huku soka letu likizidi kufa", alisema Makungu.
Aliwatoa wasiwasi wadau wa soka wenye mashaka na uamuzi huo, kwa kusema umechukuliwa kwa nia njema kwani bila ZFA yenye amani na utulivu, dhamira yake ya kukiletea maendeleo chama hicho isingeweza kufikiwa.
Aliishukuru klabu ya Miembeni kwa kufahamu dhamira yake na kukubali, pamoja na wote waliochangia kwa njia moja au nyengine kuunga mkono jitihada zake za kumaliza kadhia ya Malindi ambayo alikiri ilikuwa ikimnyima usingizi
No comments:
Post a Comment