Habari za Punde

Polisi watakiwa kutawaliwa na uadilifu


Na Ramadhan Himid, POLISI
ASKARI wa Jeshi la Polisi Zanzibar wametakiwa kufanyakazi kwa uadilifu na kufuata sheria ili kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake na watoto.

Ofisa wanawake na watoto wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mwanajuma Kassimu alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia yaliyoshirikisha askari 50 wa vyumba vya Mashitaka, Takwimu, na Askari Shehia kutoka Mikoa mitatu ya Unguja na Makao Makuu ya Polisi.

Alisema jamii haiishi kwa furaha kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na hivyo ni vyema wasimamizi wa sheria wakahakikisha kuwa jamii inaishi katika hali ya amani na usalama pamoja na kujisikia kuwa wanathaminiwa ndani ya jamii yao kwa kutofanyiwa vitendo viovu ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia.

Aidha alisema kumekuwepo kwa malalamiko mengi katika vituo vya Polisi juu ya kesi za unyanyasaji wa kijinsia kuwa hazishughulikiwi ipasavyo na hivyo kuwataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo ili iwe chachu muhimu ya kupunguza wimbi la unyanyasaji.

Ofisa huyo alisema kila mmoja aone suala la kupambana na unyanysaji wa kijinsia sio la mtu mmoja bali ni jukumu la wote na hivyo ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe kuwa anasimamia kwa karibu jambo hilo.

Awali akizungumzia lengo la mafunzo hayo ya siku tatu Mkuu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Zanzibar, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Kheriyangu Khamis, alisema lengo ni kuwajengea uwezo Askari katika shughuli hasa za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Mafunzo kama hayo tayari yameshatolewa kwa Askari wa Mikoa miwili ya Pemba wiki iliyopita na kwa sasa yanafanyika kwa Mikoa mitatu ya Unguja kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la watoto(Save the Children) na Jeshi la Polisi ikiwa lengo ni kuwajengea uwezo Askari Polisi kusimamia kesi za unyanyasaji wa kijnsia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.