Na Husna Mohammed
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, inadaiwa shilingi bilioni 1.2 na vyuo mbalimbali, ikiwa ni ada na posho za utafiti za wanafunzi wanaofadhiliwa na Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu.
Akiwasilisha hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea mjini hapa, waziri wa wizara hiyo, Ali Juma Shamuhuna, alisema deni hilo ni kwa ajili ya mwaka wa masomo uliopita.
Hata hivyo, waziri huyo alisema kwa mwaka wa masomo 2011/2012 bodi hiyo imeweza kuwateuwa wanafunzi wapya 209 sawa na asilimia 84 ili kupatiwa mikopo.
Alisema kupatiwa mikopo kwa wanafunzi hao kumefanya idadi ya wanafunzi wote waliohudumiwa kwa mikopo kwa mwaka 2011/2012 kufikia 1,086.
Shamuhuna alisema mahitaji halisi ya fedha yalikuwa ni shilingi bilioni 5.2 ambapo bodi ilitengewa shilingi 4,000,000,000 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wapya na wanaoendelea.
“Hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu fedha hizo zimeweza kupatikana zote kutoka mfuko mkuu wa Serikali, ambapo katika mwaka wa fedha 2012/2013 bodi inatarajia kupeleka masomoni wanafunzi wapya 800 kwa shahada ya kwanza na shahada ya uzamili katika vyuo vya ndani ya nchi,” alisema.
Sambamba na hilo lakini Shamuhuna alisema bodi ya mikopo iliweza kukusanya madeni ya wanafunzi ambapo jumla ya shilingi bilioni 8,200,000 zilikusanywa katika kipindi cha miezi mitatu kutoka kwa wanafunzi 71.
Hata hivyo, alisema bodi inaendelea kuwafatilia wanafunzi wengine waliokopeshwa ambao wamemaliza masomo yao ili waanze kulipa madeni yao.
Akizungumzia kuhusu kesi za ujauzito na ndoa za wanafunzi, Waziri Shamuhuna, alisema katika mwaka 2011/2012, kesi 28 za ndoa za wanafunzi ziliripotiwa ambapo kesi tatu kati ya hizo zilikuwa baina ya wanafunzi na wanafunzi na wanafunzi 18 kati ya kesi hizo 28 walifukuzwa skuli kwa mujibu wa sheria ya Elimu ya nambari 6 ya mwaka 1982 kifungu 20 (3).
Kuhusu kesi za Ujauzito, Shamuhuna alisema kesi 15 ziliripotiwa kati ya hizo kesi mbili ziliwahusu wanafunzi kwa wanafunzi, ambapo kesi tisa kati ya hizo 15 zilijadiliwa ambapo wanafunzi nane wanaendelea na masomo baada ya kukamilisha taratibu.
Aidha kuhusu elimu mjumuisho, Waziri Shamuhuna, kwa mwaka 2011/2013 kitengo hicho kimewahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu 4,500, kati ya hao wasichana ni 2,201na wavulana ni 2,299katika skuli 86 za Unguja na Pemba.
Pia alisema kitengo hicho kiliandaa upimaji wa wanafunzi na kugundua wanafunzi 696 kati ya hao wanawake 428 na wanaume 268 kuwa na matatizo makubwa na kupatiwa rufaa ya kuhudhuria hospitali kuu kwa ajili kuchunguzwa afya zao zaidi.
Waziri Shamuhuna akisema kuhusu dakhalia, alisema Wizara inakusudia kuimarisha huduma za afya katika dakahalia zote ili kufanya mazingira ya dakhalia hizo kuwa ni ya kuvutia.
Hata hivyo, alisema katika mwaka 2012/2013 jumla ya wanafunzi wanaoishi dakhalia 1,774.
Aidha Wizara hiyo inakusudia kuzifungua skuli 10 mpya za Sekondari, sambamba na kuzitumia tena skuli za Forodhani, Hamamni, Tumekuja, Uweleni, Utaani na Fidelcastro baada ya kukamilika matengenezo makubwa.
Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa shilingi 110,091,291 ,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
No comments:
Post a Comment