Habari za Punde

Waziri Hamad Masoud Kushtakiwa kesi ya Madai?




·   Ni lazima awajibike kisheria na sio kisiasa pekee
·  Wadai Wazanzibari wanaoishi nje:

Na Geofrey Kimbitikiri

Friday, 27 July, 2012.

Wazanzibari waishio nje na ambao jamaa zao walipoteza maisha yao na wengine kuathirika kiafya katika msiba wa kuzama  boti ya MV Skagit wamezungumza kwa sauti moja kutoka London, Toronto na Washington baada ya kuhojiwa na muandishi wetu na kusema kwa pamoja kuwa watampeleka aliekuwa Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Visiwani Nd. Hamad Masoud kortini kwa kile walichokiita kutowajibika na kutokufanya kazi zake sawasawa kama alivyohitajika na ile Kamati ya Rais Dr Shein ya mwanzo iliyoundwa baada ya meli ya mwanzo kuzama iliyokuwa ikielekea Pemba katika mwaka 2011.


Wameelezea Wazanzibari hao kuwa kwa wakati huu wa uwazi na ukweli, kujiuzulu kwake kulikuwa hakutoshi kwani makosa ya jinai yametokea chini ya uongozi wake.  "Kwa kweli hajawajibika bado mpaka atakaposimama mahkamani na kuwaeleza wote wale waliopoteza jamaa zao na ndugu zao kwanini meli iliachiwa kujaza watu kuliko kiwango chake." Wameelezea Wazanzibari hao kwa uchungu sana walipohojiwa kwa njia ya simu.

"Ilipozama meli ya mwanzo katika 2011 kwenye Nov-Dec mapendekezo kadhaa yalitolewa na Kamati iliyochaguliwa na Rais Dr Shein, Kamati ambayo ilikaa mawiki tele Hoteli ya Bwawani kuifanya kazi hio. 

Waziri Hamad alishindwa kuyasimamia mapendekezo hayo, yaani alishindwa kazi yake. 

Moja katika mapendekezo hayo ya Kamati ya mwanzo ni kuwa alitakiwa Waziri ahakikishe kuwa meli hazijazi abiria zaidi ya kiwango. " Waliendelea Wazanzibari hao huku wengine wakilia kwenye simu.

"Ni kweli Waziri Hamad asingeliweza kuizuwia hali ya hewa kuchafuka au kuzuwia kasi ya mawimbi ya bahari ya Chumbe, lakini kama boti ile ingelikuwa na abiria 250 tu ambao ndio kiwango chake basi msiba ungelikuwa mdogo kwa wananchi kuliko ulivyokuwa hivi sasa." Waliendelea Wazanzibari hao.

Wazanzibari hao wanakusudia kwa pamoja kupeleka Mahkama Kuu ya Zanzibar ‘a class-action lawsuit’ dhidi ya Bw. Hamad, ambayo itamtaka awalipe ndugu wa Wazanzibari wote waliopoteza maisha yao na wale walioumia kwenye hili balaa, kwasababu wanasema yeye anahusika moja kwa moja. 

Pia, wanaeleza kuwa kama Bw. Hamad angelisimamia vizuri usafiri wa meli baina ya Bara na Visiwani kama alivyotakiwa na ile Kamati ya Rais basi maafa yaliotokea yasingelikuwa makubwa hivyo.

Wazanzibari hao wanastaajabu vipi baada ya kuelezwa na Kitivo Cha Hali ya Hewa cha DSM kuwa bahari itakuwa chafu boti ndogo kama hii ya MV Skagit iliweza kuruhusiwa kuanza safari yake na huku ikiwa imechukuwa watu zaidi ya kiwango chake. “ Hii ni miradi ya wakubwa na kama boti isingelisafiri watu wangelikosa sehemu yao”, walichacharika Wazanzibari hao.


Wazanzibari hao walivyoulizwa watadai kiasi gani walipwe kwa kila aliepoteza ndugu/jamaa yake walisema kwa sauti moja kuwa ” Nia yetu sio kutafuta uchumi bali kuwapa fundisho hawa wakubwa zetu”.

Inasemekana kuwa wakati Bw. Hamad alipotolewa jela alikowekwa na SMZ (enzi za Rais Salmin Amour) alidai alipwe TShs milioni ishirini kwa kuwekwa ndani bure. 

" Sisi tunadai sio Dollar milioni moja na sio kwa kile alichokidai Bw Hamad kuwa ni kuwekwa jela bure, bali tunadai kwa maisha ya jamaa zetu yaliopotezwa bure na ambayo hayawezi kurejeshwa", walilalamika Wazanzibari hao.

“ Kama kwa kuwekwa ndani bila ya kupoteza maisha yake Bw. Hamad alidai Milono, je kwa kupotezewa maisha ya ndugu zetu bure bure tutadai kiasi gani? Bw. Muandishi utalijibu hilo suala mwenyewe”, walimalizia Wazanzibari hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe eti kwasababu lawsuit bado haijaenda Mahkama Kuu, Zanzibar.

"Waziri Hamad tokea hapo alikuwa akijipendekezesha sana kwa wale wenye kumiliki vyombo vya usafiri Visiwani", alieleza jamaa mmoja, kwa simu yake ambayo ilikuwa ikikatikakatika kila mara. " Vipi waziri mwezi mmoja nyuma alipoulizwa juu ya meli mpya ya Azam alisema eti kuwa meli hio haikuletwa kufanya faida bali kusaidia wananchi. Huu ni uwongo na inaonesha vipi waziri alikuwa anajikomba na wamiliki wa biashara za usafiri hapa Visiwani".

"Hawa wote ni wanyonyaji na wanajaza abiria kwenye meli/boti zao kama dagaa na waziri anasema eti nia yao sio kupata faida." Alieleza huyu Mzanzibari mwenye simu mbovu, huku akionesha hasira kwenye matamshi yake.

"Ni lazima waziri Hamad afikishwe kortini kujibu hoja za wananchi, kama sio hivyo mawaziri siku zote watakuwa wanatumaliza na baadae wanajiuzulu tu" Alinena Mzanzibari mwengine kwenye simu kutoka nje.


Wachunguzi wa siasa wanasema kama hii class-action lawsuit itapelekwa Mahkama Kuu huko Zanzibar basi labda itakuwa ni onyo kwa wale wote wanaopewa madaraka nchini

Chanzo: Wagagagigikoko News Network ( Wanene)

4 comments:

  1. Hawa jamaa wanataka kumshitaki Hamad Masoud au waziri wa Mawasiliano? Sasa Hamad Masoud anawajibika vipi? Pili niwaulize Hamad Masoud angeweza vipi kudhibiti idadi ya abiria wanaotoka Dar kuja Zanzibar?
    Hawa jamaa wanahitaji kumshitaki mmiliki wa meli na sio Hamad Masoud. Vyenginevyo naona wanajisumbua na kutaka kusumbua watu tu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hamad Masoud anahusika kikamilifu na ajali ya Mv Skagit kwakuwa kama waziri ameshindwa kutoa mapendekezo yoyote juu ya udhaifu na kasoro za vyombo viliopo hasa ukitilia maanani kuwa,kuzama kwa mv Skagit hakuhusiani kabisa na wingi wa abiria na mizigo bali ni kutokana na meli yenyewa kutokuwa na muundo unaoruhusu meli hiyo kuelea kwenye bahari ya wazi.akiwa Waziri, baada ya ajali ya mwanzo iliyouwa abiria waliokuwa wakielekea Pemba alitakiwa afanye utafiti wake mwenyewe na achukuwe hatuwa au kama hatua hizo zilikuwa nje ya mamlaka yake basi alilazimika kutowa mapendekezo kwa serkali,Kipenzi chenu Hamad,hakufanya hivyo.kwa hoja hiyo,tunamhesabu kuwa muuwaji kama wauwaji wengine na ni waziri mzembe kama wazembe wengine.

      Delete
  2. Kwanza, inabidi niwapongeze hawa ndugu zetu wanaoishi nje na ambao waliguswa na huu uzembe wetu hapa ZNZ. Hichi wanachokionesha ni muamko wa aina ya pekee na kama Wazanzibari leo tumefikia kuwa na muamko kama huu basi daima tutasonga mbele. Nimefurahishwa na maneno ya hawa Wazanzibari wa nje waliosema kuwa kujiuzulu sio kujiwajibisha. Haitoshi waziri aliefanya makosa ajiuzulu tu na ndio iwe imekwisha.
    Nd. Anonymous sijui kama unajua chochote kuhusu kile wanachozungumza hawa Wazanzibari wa nje. Ikiwa hujui Hamad Masoud awajibike vipi basi hii ni kweli hujui kitu. Halafu, eti unauliza Hamad Masoud angedhibiti vipi idadi ya watu kwenye boti? Ndugu yangu bora kwanza rejea darasani kabla hujaja kujiaibisha hapa ukumbini. Hivyo unajua kuwa Hamad Masoud alikuwa waziri wa Mawasiliano? Bila ya wasiwasi wowote ule hujui hivyo. Labda unadhania yeye alikuwa mkurugenzi tu!

    ReplyDelete
  3. Ndugu zangu, majibu rasmi naona yametolewa na ndugu zetu waliopo nje. Someni majibu yao hapa:

    Msimamo wao unatia moyo!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.