JENGO jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, linatarajiwa kuchukua abiria 800 wa kuingia na kutoka mara baada ya kukamilika kwake.
Meneja wa Ufundi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar, Mzee Abdalla Mzee, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari vilivyofika katika kiwanja cha kimataifa cha ndege Zanzibar, kwa ajili ya kupata maelezo juu ya ujenzi wa kiwanja hicho.
Hata hivyo, Meneja huyo alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwake wataangalia uwezekano wa kuona kiwanja hicho kutumika kwa wageni pekee au mchanganyiko.
"Tutaangalia uwezekano kama tutumie kwa wageni pekee na wenyeji watumie ule wa awali au la", alisema.
Aidha alisema kwa mwaka wanakusudia kuchukua abiria milioni 1.1 kwa mwaka kutoka nchi mbalimbali duniani.
Meneja huyo alisema jengo hilo litakuwa la kisasa ambalo litakuwa na ubora kama viwanja vyengine duniani.
Jengo hilo jipya la abiria limeanza ujenzi wake mwaka 2010 na kukamilika mwaka 2013, ambapo litagharimu dola milioni 70.4 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya EXIM.
Ujenzi huo unajengwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group ya China.
No comments:
Post a Comment