Na Mwandishi wetu
WAKUU wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC-SARPCCO, wanatarajiwa kukutana Zanzibar, kujadili na kuweka mikakati itakayosaidia kukabiliana na uhalifu wa kiamataifa ukiwemo ule unaovuka mipaka.
Mratibu wa mkutano huo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Shirikisho la Polisi wa Kimataifa Duniani (INTERPOL) nchini Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustavus Babile alisem mkutano huo wa siku tatu ambao utafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao, utatanguliwa na mikutano mingine midogo midogo ya kamati tendaji kutoka nchi wanachama.
Kamanda Babile alisema maandalizi ya mkutano huo utakaoanza Septemba 3 hadi 5, mwaka huu, yapo katika hatua za mwisho na kwamba tayari Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi 11 kati ya 14 wanachama wa Shirikisho hilo wamethibitisha kushiriki.
Alisema wakuu wa Majeshi ya Polisi waliothibisha kushiriki katika mkutano huo ni kutoka Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Swaziland, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Congo DRC, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.
Alifahamisha kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Angola, Kamishna Jenerali Ferire Do Santos Ambrosio De Lemos, ameahidi kutuma mwakilishi kwenye mkutano huo kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na uchaguzi mkuu.
Kamanda Babile alisema ofisi yake inaendelea kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Mauritius, Kamishna Jenerali Rampersad Dhun ili kuthibitisha ushiriki pamoja na wajumbe wengine wanaopaswa kuwepo kwenye mkutano huo.
Mbali ya Wakuu hao wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za SADC, pia Kamanda Babile aliwataja wajumbe wengine wanaopaswa kuwepo kwenye mkutano huo kuwa ni pamoja na Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka nchi wanachama ambao nao watawaongoza wataalamu viongozi wa vitengo mbalimbali vya majeshi Polisi kutoka katika nchi shiriki.
Wataalamu hao ni pamoja na wakuu wa vitengo vya sheria, wakuu wa mafunzo, wakuu wa mitandao ya wanawake, wakuu wa maabara ya uchunguzi wa vielelezo, wakuu wa udhibiti wa silaha ndogondogo na za rashasha, wakuu wa vikosi vya afya na utabibu, wakuu wa mifumo ya kompyuta pamoja na wakuu wa vitengo vya Interpol kutoka kila nchi wanachama.
Alisema pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo pia watajadili, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na hatimaye kubuni mikakati ya pamoja itakayosaidia kukabiliana na makosa yenye athari kwa maisha ya binadamu na yale yanayodhoofisha nguvu za kiuchumi kwa nchi za Kiafrika na duniani kwa ujumla.
Aliyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na ugaidi, uharamia, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya dawa za kulevya, makosa ambayo alisema yana athari za moja kwa moja kwa binadamu.
Aliyataja makosa yanayothoofisha nguvu za kiuchumi duniani ambayo pia yatajadiliwa kwenye mkutano huo kuwa ni ya hujuma na wizi wa fedha kutoka kwenye mabenki na taasisi nyingine za kifedha unaofanywa kwa kutumia mifumo huru ya kompyuta.
Makosa mengine ni ya wizi na usafirishaji wa magari na mifugo kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa magendo pamoja na uwekezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi itokanayo na fedha za biashara haramu.
Kamnda Babile alisema mambo mengine yatakayofanyika wakati wa mkutano huo kuwa ni pamoja na uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa shirikisho hilo la SARPCCO ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta Jenerali Saidi Ali Mwema, anapewa nafasi kubwa ya kushika wadhifa huo baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini Kamishna Jenerali Mangwashi Phiyega, kumaliza muda wake katika nafasi hiyo.
Kamanda Babile alisema endapo IGP Mwema, atachaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Shirikisho hilo la SARPCCO, itakuwa ni mara ya pili kwa Jeshi la Polisi nchini Tanzania kushikilia tena nafasi hiyo kubwa ya Mashirikisho ya Kimataifa Duniani.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilipata nafasi hiyo mwaka 2004 na 2005 kupitia kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta Jenerali Mstaafu Omari Iddi Mahita.
IGP Mstaafu Mahita, aliweka historia ya kuwa Mkuu wa kwanza wa Jeshi la Polisi hapa nchini kuwaongoza Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika kupitia Shirikisho hilo kubwa la (SARPCCO) tangu lilipoanzishwa mnamo mwaka 1995, katika mji wa Swakompumg nchini Namibia.
No comments:
Post a Comment