Habari za Punde

BOT yatoa futari kwa jirani zake Gulioni

Na Mwashamba Juma
BENKI Kuu ya Tanzania (BOT), tawi la Zanzibar juzi ilikabidhi vyakula kwa ajili ya futari vyenye thamani ya shilingi 550,000 kwa wananchi wa shehia ya Gulioni iliyopo mjini hapa.

Kaimu Mkurugenzi wa tawi hilo Nicodemus Mboje, alikabidhi vyakula hivyo vya futari kwa sheha wa shehia ya Gulioni, Mwantum Hilal Mzee, ambayo iko karibu na Ofisi Kuu ya BOT tawi la Zanzibar.

Miongoni mwa vyakula vilivyotolewa kwa wananchi wa Gulioni ambapo ndipo zilizopo ofisi benki hiyo, ni pamoja na mchele, unga wa ngano, sukari na mafuta ya kupikia.

Akikabidhi vyakula hivyo Kaimu huyo alisema benki yake inaungana na wananchi wa Gulioni pamoja na waislamu wote kwa ujumla katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Benki kuu ya Tanzania tawi la Zanzibar inaungana na majirani zake katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni ishara ya kudumisha ujirani wetu” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Alisema funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ambayo ni nguzo ya nne katika dini ya kiislamu ni wakati mzuri kwa watu kusaidiana jambo ambalo ndilo lililoisukuma benki hiyo.

Aidha Mboje aliwatakia mfungo mwema wananchi wa Gulioni na waislamu wote pamoja na kuwatakia kila la kheri katika kuadhimisha sikukukuu ya Eid el Fitri.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Gulioni, Mwatum Hilal Mzee, aliishukuru benki hiyo kwa msaada huo na kueleza kuwa utawafika walengwa.

Alisema shehia yake inathamini sana msaada huo uliotolewa na benki na kutaka uwepo ushirikiano mwema baina ya taasisi hiyo na wananchi wa Gulioni kwa ujumla.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.