Na Kunze Mswanyama, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), amewaomba radhi waisalamu waliosumbuliwa na takwimu zisizo za ukweli zilizotolewa na kituo siku ya sherehe za muungano huku pia akisema tayari wamekwishamshughulikia muhusika wa kadhia hiyo.
Aprili 26 mwaka huu katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, mchanganya picha wa kituo hicho alitoa takwimu zilizokuwa zikionesha kuwa nchini Tanzania kuna wakristo 52%,waislamu 32% na wapagani 14% jambo ambalo si kweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana alisema kuwa takwimu hizo walizipata toka kwenye mtandao wa wikipedia ambazo pia hazikuthibitishwa na Idara ya Takwimu ya Taifa (NBS).
Kwa mujibu wa sheria, hapa nchini ni NBS pekee wanaoruhusiwa kutoa takwimu ambazo huweza kutumika kwa shughuli mbalimbali halali.
Alieleza kuwa takwimu hizo zimewaudhi waislamu hapa nchini na kujikuta wanalimwa barua ya kutakiwa kuomba radhi na Jumuiya ya wanataaluma wa kiislamu Mei mwaka huu.
Siku hiyo ambayo pia kituo hicho kilionesha jinsi jina Tanzania lilivyozaliwa na Waasisi wawili nguli wa taifa hili Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume mwaka 1964, takwimu hizo zilioneshwa mara moja tu.
“Nawaomba radhi wale wote waliokwazika na takwimu hizo, wakumbuke kuwa mwezi huu ni wa toba hivyo watusamehe sana kwani tumeomba radhi kwa maneno, barua, TBC live na sasa kupitia vyombo mbalimbali vya habari”, alisema Mshana huku akiwasihi wananchi wote kutoa ushirikiano kwa maofisa wa sensa ijayo.
Alisema, shughuli za sensa ni muhimu kwa kila mmoja ambapo serikali pia huzitumia kugawa shughuli za maendeleo na kuwa kila huduma hupelekwa kulingana na idadi ya watu wanaopatikana kwenye eneo husika.
Aliongeza kuwa, hiyo ni changamoto kubwa kwao kutokana na baadhi ya mambo kujikuta yanawaudhi wadau wao ambao ndiyo watazamaji huku wao wakidhani ni kuboresha huduma hiyo muhimu.
Aliwaasa waandishi wote nchini wanaopenda kutumia takwimu kuhakikisha kuwa wanazipata kutoka kwenye mamlaka husika ili kuondoa utata kwani takwimu hizo walizozionesha mara moja tu zimewaudhi watu wengi nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari huzi jijini Dar es salaam, Katibu wa Shura ya Maimamu Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema takwimu hizo zilizotolewa na TBC kuwa zimewachanganya na kuitaka serikali kuwahesabu upya waumini wa dini zote ili kupata taarifa kamili.
Siku ya sensa ya watu na makaazi itafanyika Agosti 26, itawahusisha watu wote watakaokuwea wamelala usiku wa Agosti 25 nchini ili kupata idadi ya raia na wageni wote waliopo nchini.
Sensa hiyo itakuwa ya tano tangu kuanzisha kwa taifa la Tanzania ambalo limeundwa na nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment