Omar Abdallah na Asha Abdallah, ZJMMC
WAANDISHI wa Habari na Makamanda wa vikosi vya ulinzi na usalama wa Mkoa wa Kusini Pemba, wametakiwa kutumia nafasi zao juu ya kuwaelimisha wananchi katika suala zima la sensa ili kuweza kufikia lengo hilo.
Akitoa agizo hilo waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili ya Rais Mohamed Aboud katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, alisema waandishi na makamanda wanayo nafasi kubwa ya kuwaelimisha wananchi juu ya zoezi hilo.
Alisema kuwa kushiriki katika zoezi hilo ni njia moja wapo ambayo itaiwezesha serikali kupata takwimu sahihi na taarifa nyengine ambazo ziatairahisishia pale endapo wakitaka kuwaletea maendeleo wanachi wake.
Alieleza suala la sensa lipo kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi hivyo sio busara kujitokeza kwa baadhi ya mkundi ya watu na viongozi kuwataka wananchi wasusie kwa zipo faida kadhaa ya zoezi hilo.
Akitaja miongoni mwa faida ya zoezi hilo la sensa ya watu na makaazi ni kumuwezesha mwananchi kupata kitambulisho cha mtanzania, vitambulisho vya kupigia kura na hata juu ya suala la kupata pasi za kusafiria.
“Wengi wa wananchi wetu wanadhani kuwa zaozi hilo halina maana, hivyo ni wajibu wenu waandishi wa habari na makamanda wa vikosi vya Ulinzi na usalama kuwaelimisha wananchi na wafanyakazi wao’’, alifafanua Waziri Aboud.
“Mwananchi yeyote ambaye atakataa suala zima la sensa ya watu na makaazi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, na vyombo vya habari vitakavyopotosha juu ya zoezi hilo kuvifungia”, alisema Aboud.
Nae Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, Juma Kasim Tindwa alisema kuwa kila baada ya miaka 10 Serikali hufanya zoezi kama hili kwa lengo la kujua idadi ya wananchi wake ili iweze kujipanga katika mikakati yake ya maendeleo sambamba na kupunguza umaskini na kukuza uchumi.
Hata hivyo aliwataka wananchi wasiingize itikadi za kidin wala siasa katika zoezi hilo la sensa ya watu na makaazi, na kuwataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo linalotarajiwa kuanza Augosti 26 mwaka huu nchini kote.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hassan Nassir alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi wanakataza suala la sensa lakini kupitia vikosi vya ulinzi wanafanya jahudi kubwa ili kuwaelimisha wananchi kupitia kwa vikosi vya polisi jamii.
No comments:
Post a Comment