BAADHI ya masheha wameonyesha wasiwasi wao juu kusahaulika kwa watu kwenye zoezi la sensa ya watu na makaazi inayoendelea nchini kote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, masheha
hao walisema, wakati zoezi hili likiingia siku ya sita, zipo baadhi ya kaya
ambazo hazijafikiwa na makarani wa sensa, hali inayowatia hofu huku zoezi hilo
likiwa linaelekea kukamilika siku ya Jumamosi.
Sheha wa Pangawe wilaya ya Magharibi Unguja,
Abdallah Juma Mtumweni, alisema, kumekuwepo na maeneo ambayo hadi sasa zoezi
hilo halijafanyika kutokana na kuwepo kwa makarani wachache kwenye maeneo hayo.
Aliyataja maeneo hayo ni pamoja na Fuoni
Mambosasa ambako idadi kubwa ya kaya hazijahesabiwa na kwamba wananchi
wanaendelea kutoa ushirikiano na uongozi wa shehiya kuhakikisha wanafikiwa na
makarani hao.
Hata hivyo, alisema, pamoja na kasoro hiyo
ndogo, zoezi la sensa linaendelea vizuri kwenye shehiya hiyo, ingawa zilikuwepo
changamoto nyengine wakati wa kuanza kwa zoezi hilo.
"Yupo karani ambaye aliibiwa kabrasha
lake la sensa, lakini huyu muhalifu alitiwa mikononi na jeshi la polisi na
taratibu za kisheria zinaendelea", alisema Mtumweni.
Naye sheha wa Tomondo, Mohammed Omar
Said, alisema, wapo baadhi ya watu
katika shehiya hiyo wanaoendelea kugomea zoezi hilo sambamba na kubandikwa kwa
vipeperushi vyenye kutoa vitisho kwa wananchi wengine juu ya zoezi hilo la
kitaifa.
"Ipo nyumba iliyobandikwa tangazo la
kutishia makarani, lakini uongozi wa shehiya umeshalifanyia kazi suala
hilo".
Alisema, watu wanagomea zoezi hilo
wanaendelea kutoa sababu za kidini wakitaka kupata kauli kutoka kwa masheikh
wao kabla ya kushiriki zoezi hilo.
Sheha wa Fumba, Issa Hassan Shoka, zoezi
linaendelea vizuri huku baadhi ya watu
wakiwagomea makarani wanaofika kwenye kaya zao ikiwa pamoja na kutoa lugha za
matusi kwa makarani hao.
"Tulijaribu kuwaelemisha watu hawa
umuhimu wa zoezi la sensa, lakini hatimaye walituelewa na kutoa ushirikiano kwa
makarani", alisema Shoka.
Mapema Mkuu wa wilaya ya Magharibi, Hassan
Mussa Takrima, aliwataka wananchi kutumia vizuri fursa hiyo huku wakielewa zima
kubwa inayowakabili katika kuleta maendeleo ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Sensa ya idadi ya watu na makazi ilianza
nchini kote usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu ambapo Watanzania wote bila
kujali itikadi za vyama, dini ama kabila wametakiwa kushiriki kikamilifu zoezi
hilo la kitaifa.
No comments:
Post a Comment