Habari za Punde

Ajali ya kutisha. Wanane wafa, wamo wanafunzi wanne


Na Mwandishi wetu, Pwani
WATU wanane wakiwemo wanafunzi wanne wa shule ya sekondari Msolwa wamekufa baada ya magari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na fuso katika eneo la Kibiki  tarafa ya Chalinze mkoani Pwani.

Ajali hiyo iliyotokea saa 12 :20 jioni iliyahusisha magari yenye namba za usajili  T.363 AZG, Toyota mark II lililokuwa likiendeshwa na  Abuu Ahmedi (21)  na fuso lenye namba za usajili T.433 AYQ lililokuwa likiendeshwa na Mweta Daniel (40).

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani,Gregory Mushi  alisema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya dereva wa fuso kushindwa kulidhibiti gari lake na kupoteza mwelekeo kisha kuligonga gari dogo.

Kamanda Mushi aliwataja watu waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni  Esau Enos (16) ambae ni mwanafunzi wa kidato cha tatu, Bahati George (18), mwanafunzi wa kidato cha nne,Latifa Maneno Shabani (17), mwanafunzi wa kidato cha nne,Stela Issack Kazimoto (18) wanafunzi wa kidato cha tatu na Hassani Kulunga  ambae umri wake bado haujafahamika.

Wengine ni  Maria Sadiki Lelela, Samwel Ismail,   miaka 3 – 4 na  Abuu Ahmed (21) ambaye alikuwa dereva wa gari dogo.

Aidha alisema ajali hiyo ilisababisha majeraha kwa abiria waliokuwa katika fuso ambao ni  William Tobias (30) na Ahmada Ahmada Juma (36), aliyekuwa utingo wa fuso hilo na wanaendelea na matibabu katika kituo cha afya Chalinze na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitali ya teule ya Tumbi Kibaha.   

Kamanda Mushi alitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali za kizembe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.