Habari za Punde

Hofu ya kuambukizwa HIV yatanda. Wenye virusi wadaiwa kusambaza kwa makusudi


Na Masanja Mabula, Pemba
BAADHI ya wanachama wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Kisiwani Pemba wamedaiwa kuendelea kueneza virusi vya Ukimwi kwa makusudi licha ya kujitambua kuwa wanaishi na maambukizi ya ugonjwa huo, hali iliyowapa hofu kubwa wananchi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Wete, Katibu wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar, Saade Said Saduni alisema hali hiyo inakwamisha kufanikisha lengo la serikali la kupunguza maambukizi mapya katika jamii.
Alisema jumuiya hiyo kisiwani  Pemba imepokea taarifa hizo kutoka kwa wananchi na kwamba wanaendelea kuzifanyia kazi na kuongeza kwamba upelelezi wa awali umeonyesha kuwepo uenezaji wa virusi hivyo kwa makusudi kunakofanywa na wanachama wa jumuiya hiyo.

"Taarifa hizi tunazo na tunazifanyia kazi , kwani tumezipokea kutoka kwa wananchi na baada ya kufanya ufuatiliaji wa awali tumebaini kuwepo na ukweli ndani yake, lakini wacha tuendelee kufanya uchunguzi zaidi, " alifahamisha.
Aidha Saade amefahamisha jumuiya hiyo haiwezi kuvifumbia macho vitendo hivyo ambavyo vinaweza kuleta athari zaidi kwa jamii kutokana na kwamba maambukizi mapya yanaweza kuongezeka.
Katika hatua nyingine Saade amewataka viongozi kuanzia ngazi za shina hadi taifa kuendelea kushirikiana na ZPHA+ katika kutoa elimu kwa jamii ili kuona kwamba elimu hiyo inaleta faida kwa wanajamii.
Alieleza  kwamba kwa sasa ushirikiano kutoka kwa viongozi hao haupatikani kutokana na viongozi hao kushindwa kuendelea kutoa elimu ya Ukimwi baada ya wafadhili waliokuwa wakifadhili kamati za ukimwi kusitisha misaada yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.