Habari za Punde

Mbuzi 31 walikufa Matemwe kwa ugonjwa wa baridi



Na Mwashamba Juma
MBUZI 74 walikumbwa na maradhi ya baridi katika kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja katika kipindi cha kuanzia  mwezi Disemba  mwaka jana na Januari mwaka huu, ambapo kati yao mbuzi 31 walikufa.
Mkurugenzi Idara ya huduma za utabibu wa mifugo Zanzibar, Dk. Yussuf Haji Khamis, alisema mwezi Disemba mbuzi 54 waliugua ugonjwa huo na mbuzi 17 walifariki.
Alisema kwa mwezi Januari mbuzi 20 waliugua, ambapo mbuzi 14 walikufa.
Mkurugenzi huyo alisema tayari wametuma timu ya madaktari bingwa wa mifugo katika Wilaya ya Kaskazi hasa katika maeneo ya Matemwe, Pwani Mchangani na vijiji jirani kwenda kufanya uchunguzi wa kina.

Aliwataka wafugaji wilayani humo kujenga mabanda kwa ajili mifugo yao ili kuwanusuru na maradhi pamoja na kuwataka kuvitumia vituo vya afya  hasa wanapogundua matatizo ya mifugo yao.
Kuhusu taarifa za kuwepo maradhi ya nyimonia ambayo kitaalamu yanajulikana kama Contagious Caprine Pleuro Pneumonia (CCPP), Mkurugenzi huyo alisema bado hawajathibitisha kuwepo maradhi hayo
Kwa mujibu wa utafiti mgodo walioufanya mara baada ya kupokea taarifa za kuwepo kwa maradhi hayo, Dk. Yussuf alisema waliamua kuchukua mbuzi aliekufa na kumfanyia uchunguzi kupitia mapafu, figo, damu, maini na kinyesi, chake, na kubaini kuwa baridi kali iliyopo katika maeneo wanaofugwa mbuzi hao ndio chazo cha mbuzi hao kufa.
“Tatizo la wafugaji wa Matemwe hawajengi mabanda kwa ajili ya mifugo yao ukiangalia wapo karibu na ukanda wa bahari, hivyo mwanyama wengi wanaathiriwa na baridi kali hasa nyakati za usiku hali inayowasababishia wanyama hao kuugua mara kwa mara,” alisema Mkurugezi huyo.
Dk. Yussuf pia alipinga kuwepo kwa taarifa za watu kula mizoga na kusema kuwa Wizara yake haijapokea wala kuwa na taarifa hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.