Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali imefanikiwa kupata miradi ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi kwani kuna wawekezaji watawekeza katika viwanda vya uvuvi na shughuli za uvuvi katika bahari kuu.
Dk. Shein, aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi baada ya kufungua soko la samaki katika diko la Mazizini mjini Zanzibar.
Alisema wawekezaji hao wamo katika mazungumzo ya mwisho na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi (ZIPA) ili kuanza kazi jambo ambalo litasaidia kukuza sekta ya uvuvi.
Alisema Zanzibar itatekeleza miradi hiyo kwa vile bado sehemu kubwa ya bahari yake haijatumika kutokana na wavuvi wengi kutokuwa na zana za kuvulia katika bahari kuu.
Alisema dunia imekuwa ikivua kitaalamu jambo ambalo Zanzibar haijaweza kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na vifaa vya kisasa vinavyowawezesha wavuvi kulifikia eneo la bahari kuu.
Alisema wakati akiwa anaomba kura aliahidi atahakikisha Zanzibar itaingia katika mapinduzi ya kilimo na uvuvi jambo ambalo serikali imeanza kulitekeleza kwa vitendo.
Alisema kuwepo uwekezaji huo kuitaifanya Zanzibar kuingia katika mabadiliko makubwa ya uvuvi wa uvunaji wa samaki katika mabwawa.
Dk. Shein, aliwataka wananchi kutambua njia za kupata masoko ya samaki kwa kuwa hivi sasa wanauzwa kienyeji zaidi.
Alisema inawezekana hali hiyo imekuwa ikijitokeza kutokana na ukosefu wa masoko katika baadhi ya maeneo na uamuzi wa serikali kujenga masoko una lengo la kuondoa tatizo hilo.
Aliwapongeza wananchi na viongozi wa TASAF na Wizara ya Uvuvi kwa kuhakikisha mradi huo wa soko unafanikiwa baada ya wananchi kuukubali kwa kutoa michango yaliyofikia shilingi 1,000,000.
Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdilahi Jihad Hassan, akitoa maelezo yake alisema kujengwa kwa soko hilo kutaweza kusaidia kupunguza tatizo la athari za kimazingira katika eneo hilo.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Dk.Kassim Gharib, alisema mradi huo umetumia milioni shilingi 29.6 na litatumiwa na wavuvi 35,000.
Mbunge wa Jimbo la Kiembesamaki, Waride Bakari Jabu, aliipongeza serikali kwa jitihada ilizozichukua kujenga soko hilo.
Dk. Shein pia alitembelea mradi wa wa njia ya ya kutulia ndege na maegesho katika uwanja wa ndege Zanzibar na kukuta changamoto mbali mbali katika uwanja huo.
Mradi mwengine alioukagua ni wa mboga mboga wa uliopo Kombeni wilaya ya Magharibi Unguja, kiwannda cha matofali na kuangalia athari za uchafuzi wa mazingira katika eno la Kwarara.
No comments:
Post a Comment