Na Ameir Khalid
KAMATI ya Mifugo, Utalii na Uwezeshaji ya Baraza la Wawakilishi, imetembelea Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi Zanzibar, na kupokea taarifa ya utendaji kutoka kwa uongozi wa chuo hicho.
Akiwasailisha ripoti hiyo mbele ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Asha Bakari Makame, Mkurugenzi wa chuo hicho,Zulekha Kombo Khamis alisema katika kipindi hichi chuo kilijipangia kutekeleza mikakati mbali mbali ambayo baadhi yao imeweza kutekelezwa, licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi.
Alisema hadi sasa jumla ya wanafunzi 2,725 tayari wamepatiwa mafunzo mbali mbali ya yanayohusiana na utalii katika ngazi ya cheti na stashahada, ambao baadhi yao wameajiriwa katika hoteli za kitalii na wengine wamejiajiri wenyewe.
Akitaja baadhi ya malengo waliyojipangia na kufanikiwa kuyatekeleza ni pamoja na kuimarisha uhusiano na mashirika mengine ya kitalii, pamoja na kuwahamasisha vijana na kupenda utalii, kwa kutekeleza dhana ya utalii kwa wote.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa pia wameweza kuimarisha ujenzi wa majengo ambapo hivi karibuni wanatarajia kuyafungua.
Aidha katika malengo hayo wamefanikiwa kuwapeleka wafanya kazi saba katika vyuo mbali mbali, ndani na nje ya nchi, kusomea fani mbali mbali kwa lengo la kuongeza idadi ya wafanya kazi wenye elimu ndani ya chuo.
Mbali na mafanikio hayo, Mkurugenzi huyo alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ucheleweshaji wa malipo kwa baadhi ya wanafunzi ambapo wakati mwengine hufika hatua ya kuwazuilia mitihani yao, hali ambayo haitoi taswira nzuri kwa wanafunzi na uongozi wa chuo.
Alisema kuwa pia wamekuwa na ushirikiano mdogo kwa baadhi ya wamiliki wa hoteli katika kuwapokea wanafunzi wao ikiwemo hoteli ya Serena, ambao imekuwa ikigoma kupokea wanafunzi wa chuo hicho, ukosefu wa gari ambapo hivi sasa wanatumia gari moja ambayo nayo haipo katika hali nzuri.
Mbali na hayo pia alibainisha kuwa tatizo kubwa ambalo linawakabili ni kukosa takwimu sahihi za wanafunzi ambao tayari wamepata ajira katika sekta ya utalii.
No comments:
Post a Comment