Na Khamisuu Abdallah
WIZARA ya Kilimo na Maliasili Zanzibar imesisitiza nia yake ya kuendelea kupiga marufuku uingizaji wa migomba na ndizi kutoka nje ili kupunguza uwezekano kuenea ugonjwa wa migomba.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa wa kitengo cha utabibu wa mimea na ukaguzi mazao Zanzibar, Mustafa Abdalla Hassan, kufuatia kuwepo taarifa za kuzuka maradhi ya migomba katika baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Mwanakwerekwe, Afisa huyo alisema wizara yake imewaagiza wakaguzi wa kilimo nchi nzima kusimamia suala hilo kuhakikisha miche ya migomba na ndizi kutoka nje haziingizwi nchini.
Aidha alisema uingizwaji wa miche ya migomba na ndizi kutoka Tanzania Bara na maeneo mengine umepingwa karantini toka mwaka 2010 kutokana na kugundulika kwa maradhi hatari yatokanayo na miche hiyo.
Hata hivyo, alifahamisha kuwa ukaguzi zaidi huwekwa katika bandari za Zanzibar kama vile Mkokotoni, Malindi na uwanja wa ndege na hata katika masoko ambapo hupelekwa bidhaa hizo kwa uuzwaji kwa wananchi.
Hivyo alitoa ushauri kwa wakulima, wanapoomba miche kwa wakulima wenzao kuwaita maafisa wa kilimo kuikagua kwanza kabla ya kuipanda.
Nae Mkaguzi, Khamis Mohammed Khamis kutoka wilaya ya Kaskazini ‘B’ alisema muingizaji yoyote wa bidhaa kutoka Tanzania Bara lazima awe na kibali ambacho kinaonesha mazao hayo yameshakaguliwa na yapo safi ndio anaruhusiwa kuingiza nchini.
No comments:
Post a Comment