Habari za Punde

Sita wafanyiwa upasuaji saratani ya koo Mnazimmoja

Na Madina Issa
MADAKTARI bigwa wa hopsitali kuu ya Mnazimmoja wamefanya upasuaji wa saratani ya koo kwa wagonjwa sita waliokuwa wakisumbuliwa ugonjwa huo kwa muda mrefu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, madaktari hao walisema upasuaji huo ulifanikiwa vizuri ambapo wagonjwa hao kwa sasa wapo katika hali nzuri baada ya sauti zao kurudi katikahali ya kawaida.

Dk. Naufal Kassim Mohammed ambae ni mmoja ya madaktari walioshiriki katika upasuaji huo, akishirikiana na Dk. Mwanana Kassim Ali, walisema wagonjwa hao walifika hospitali hivi karibuni kuangalia afya zao na baada ya kuchunguzwa waligundulika kuwa na saratani ya koo.

Dk. Naufal alisema, upasuaji ulifanikiwa vizuri na wagonjwa hao sasa watalazimika kufika hospitali kila baada ya kipindi kufanyiwa uchunguzi.

Alisema saratani ya koo inaenea kwa kasi kubwa miongoni mwa wananchi.
Alisema moja ya dalili zake ni kupotea sauti hivyo amewashauri wananchi walio na dalili hizo kufika hospitali kufanyiwa uchunguzi.

Alisema ugonjwa huo chanzo chake bado hakijajulikana ila matibabu yake ni mgonjwa kufanyiwa upasuaji.

Hata hivyo, alisema inawezekana ugonjwa huo unasababishwa na uvutaji sigara na unywaji wa pombe.

Madaktari hao wameitaka jamii kuwa na mwamko wa kwenda kupima afya zao kwani hivi sasa watu wengi wamekuwa wakidharau magonjwa katika hatua za awali ambazo ugonjwa unaweza kutibika.

Nae mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji,Ali Mohammed Aboud mkaazi wa Chukwani alisema chanzo cha ugonjwa huo alianza kukauka a sauti na baada ya kwenda hospitali aligundulika kuwa na saratani ya koo.

Hata hivyo, alisema kwa sasa anajisikia vizuri na anaendelea kufanya vipimo mbalimbali na hata sauti yake inatoa vizuri.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.