Habari za Punde

Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri ashambuliwa. Apelekwa Sauzi kutibiwa. Waandishi Zanzibar walaani

Na Waandishi wetu, DSM
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Dimba na Bingwa, Absalom Kibanda amevamiwa na watu wasiojulikana wakati akiingia nyumbani kwake maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Kibanda alivamiwa majira ya saa sita usiku wa kuamkia jana, akitokea kwenye majukumu yake ya kila siku.

Inadaiwa kuwa alichomolewa kwenye gari, akapigwa kwa kutumia vitu vyenye ncha kali kichwani.

Habari zinasema Kibanda ametobolewa jicho lake la kushoto pamoja na kunyofolewa kucha na baadhi ya vidole na baadae kutupwa umbali kidogo wa nyumbani kwake.

Baadae wasamaria wema walijitokeza na kumkimbiza hospitali ya taifa Muhimbili, ambako alipokelewa vizuri na madaktari na kupatiwa matibabu ya awali.

Baadaye alihamishiwa taasisi ya tiba ya mifupa (MOI) ambako anaendelea na matibabu.

Watu waliomshambulia Mwenyekiti huyo hawakuchukua kitu chochote ndani ya gari lake ingawa kulikuwa na laptop, simu na nyaraka nyengine.

Polisi imesema inaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari waliojitokeza kwa wingi kumjulia hali katika chumba cha wagonjwa wa uangalizi maalum (ICU) alikolazwa,Kibanda alisema hafahamu kwa nini amevamiwa na watu hao ikiwa ni saa chache kabla hajapanda kizimbani kuendelea na kesi yake ya uchochezi iliyokuwa ikitarajiwa kuendelea jana katika mahakama ya Kisutu.

Alisema, alikwishaliarifu zamani jeshi la polisi kuhusiana na kutishiwa maisha na watu asiowafahamu ambapo jeshi hilo lilipuuzia taarifa hiyo.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa TEF,Theofil Makunga,alisema wanaliacha jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kuwabaini wahalifu hao kisha kuwakamata na kuwafikisha mahakamni ili sheria ichukue mkondo wake.

Alisema,tayari wamekwishawasiliana na mwanasheria wake na mahakama ili itoe hati ya kusafiria inayoshikiliwa mahakamni hapo ili Kibanda apelekwe Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, alilisifu jeshi la polisi kwa ushirikiano mkubwa waliounesha tangu walipopewa taarifa hizo ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alikuwa nao mstari wa mbele kuhakikisha afya ya Kibanda inapiganiwa na kila mwenye dhamana yake.

Kwa upande wake Hussein Mohammed Bashe ambayeni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) inayochapisha magazeti ya Mtanzania,Rai,Dimba na The African,alisema maandalizi yote ya safari tayari na ana uhakikia leo (jana) Kibanda atasafiri kwenda Afrika Kusini kupata matibabu.

Bashe alisema,hakuna kitu kibaya kama muendelezo wa mashambulizi dhidi ya waandishi kwani kufanya hivyo ni kuuminya uhuru wa habari jambo litakalowafanya wananchi kukosa habari mbalimbali za maendeleo ya taifa.



Naye Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, ASP Advera Nsenso,ambaye alimtembelea Kibanda kumjulia hali,alisema tayari Mkuu wa jeshi hilo IGP Said Alli Mwema,ameunda timu ya wapelelezi wazoefu ambao watajihusisha pia na uchunguzi wa kimaabara ili kuwabaini wote waliohusika na kuwatia mbaroni mara moja.

"Tunaomba wananchi watupe nafasi ili timu iliyoundwa itafute majibu ya hili lakini ndani ya timu hiyo kuna wachunguzi wa kimaabara ambao ni wazoefu na tunaamini watafanya kile wanachotazamiwa, hivyo wananchi wawe watulivu tu," alisema ASP Senso.

Hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Timu hiyo ya makachero wanne kutoka makao makuu ya polisi itaunganisha nguvu na makachero wa Kanda Maalum ya Dar es salaam ili kuwabaini wahusika wote wa uhalifu huo.

Awali akizungumza muda mfupi baada ya kumjulia hali Kibanda,Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa vyombo vya habari, Dk.Reginald Mengi,alisema wao watahakikisha wanashirikiana na vyombo vya dola kuwatia mikononi wahusika wote lakini pia wakiamini kuwa chombo hicho kitatumia weledi katika kuwasaka na kuwakamata wahalifu hao.

Katika taasisi ya mifupa,simanzi zilitawala baada ya umati mkubwa wa waandishi wa habari na wahariri kujitokeza kumjulia hali Kibanda.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, aliwasili hospitali aliyolazwa Mwenyekiti huyo kwenda kumjulia hali.

Nayo Jumuia ya Wandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) imepokea kwa mshituko na masikitiko habari za kujeruhiwa Absalom Kibanda.

Jumuiya hiyo imesema inaungana na wengine katika tasnia ya habari, na watetezi wa haki za binaadamu kulaani kitendo hicho.

Katika hatua nyengine Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema Kibanda mara baada ya kufika nyumbani kwake alipiga honi ili afunguliwe geti na wakati mlinzi akijiandaa kufungua alisikia sauti ya Absalom akiomba msaada hivyo akajua kuna hatari nje.

Alisema hivyo mlinzi huyo badala kufungua mlango aliamua kwanza kuomba msaada kwa majirani ndani ya uzio ilimo nyumba ya Mwenyekiti huyo.

Alisema majirani wawili walijitokeza pamoja na familia ya Absalom pamoja na mlinzi wakatoka nje ili kutoa msaada lakini walikuta gari la mlalamikaji likiwa peke yake na mlango wa mbele kushoto uko wazi.

Alisema walikuta gari lake likiwa limeharibiwa kwa kuvunjwa vioo na yeye mwenyewe akiwa amekokotwa umbali wa mita 30 kutoka kwenye gari lake.

Taarifa nyengine zilizotufikia zinasema Kibanda tayari amepelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu.

Meneja uhusiano taasisi ya tiba ya mifupa Muhimbili (MOI), Juma Almas alisema alisafirishwa jana mchana kwenda kupata matibabu zaidi.

Wakati huo huo, Waziri wa Afya Dk.Hussein Mwinyi amepokea vifaa vya msaada kwa ajili ya kufanyia upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya vichwa kikubwa uliotolewa na serikali ya Kifalme ya Saud Arabia vyenye thamani ya dola 140,000.

Msaada huo umekuja kutokana na idadi ya watoto wenye matatizo hayo kuzidi kuongezeka ambapo hivi sasa wapo zaidi ya 4000 na wanaobahatika kufanyiwa upasuaji ni nusu tu ya watoto wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.