Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 08/04/2013
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein Jumatano ijayo anatarajiwa kuzindua Mradi mpya wa Umeme ulioanzia Rasi Kiromoni Tanzania Bara hadi Mtoni mjini Zanzibar katika sherehe zitakazofanyika Uwanja wa Amani.
Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 68.2 hadi kukamilika kwake, matayarisho yake yalianzia toka mwaka 2008 ikiwa ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafuta umeme wa uhakika kwa kisiwa cha Unguja.
Akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake Waziri wa Ardhi, Makaazi Maji na Nishati Ramadhan Abdulla Shaaban amesema Mradi huo una uwezo wa megawati 100 na utaondosha matatizo mengi ya umeme ambayo yalidumu kwa muda mrefu.
Amefahamisha kuwa kwa sasa mahitaji ya umeme kwa kisiwa cha Unguja hayazidi megawati 55 wakati umeme wa zamani ulikuwa Megawati 40 na hivyo kupelekea mgao na kukatika umeme mara kwa mara.
“Naomba Wananchi wajenge matumaini makubwa ya Umeme wa uhakika na kwamba hakutakuwa tena na mgao labda matatizo madogo madogo ya kiufundi” Alifafanua Waziri Shaaban
Ameongeza kuwa kukamilika kwa Mradi huo kutakuwa ni kivutio kikubwa kwa Wawekezaji Vitegauchumi wa ndani na nje ya Nchi kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika.
Akifafanua kuhusu kuzimika kwa umeme katika baadhi ya Mitaa Waziri Shaaban ameseme tatizo hilo halitokani na Mgao bali ni tatizo la kiufundi linalosababishwa na uchakavu wa Waya na uungwaji holela wa umeme.
“Kwa vile huu Mradi unachukua umeme mkubwa na kuna baadhi ya Mitaa nyaya zake zimechakaa sana ndiko kunakosababisha kukatika umeme katika mitaa hiyo” Alibainisha Waziri Shaaban.
Waziri Shaaban amewataka Wananchi kujitokeza kwa Wingi katika Viwanja vya Amani kushiriki sherehe hizo ambazo zitapambwa na burudani za vikundi mbalimbali vya ngoma kutoka Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja.
Mradi huo wa Umeme umefadhiliwa na Marekani kupitia Taasisi yake ya kupambana na Changamoto za Milenia (MCC) ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechangia Dola za Kimarekani Milioni 1.4 kufidia mali za Wananchi katika sehemu zilizopita Mradi wa Umeme huo.
No comments:
Post a Comment