Yaridhia hatua ya Kaburu kujiuzulu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMATI tendaji ya klabu ya Simba imeridhia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, huku ikimkatalia Zacharia Hans Poppe kuachia ujumbe waKamati ya Usajili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana makao makuu ya Simba, mtaa wa Msimbazi, Ofisa Habari wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga, amesema maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika juzi.
Aidha, Kamwaga amesema, kikao hicho kimemteua Mwenyekiti, Ismail Aden Rage kuongoza kampeni za kwenda kumbembeleza Hans Poppe abatilishe uamuzi wake wa kujiuzulu na kuendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la Simba.
“Kama utakumbuka, hata Mwenyekiti wetu, Rage alijiuzulu ujumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, lakini Kamati Tendaji ya TFF, chini ya Rais wake Leodegar Tenga ikamkatalia, hivyo si ajabu kwa Hans Poppe kukataliwa kujiuzulu”, alisema Kamwaga.
Kamwaga pia alifahamisha kuwa, hatua hiyo imeendana na uamuzi wa mkutano wa matawi uliofanyika mwezi uliopita Dar es Salaam, ambao ulikubali kujiuzulu kwa Kaburu, lakini ukakataa Hans Poppe kuondoka.
Ofisa Habari huyo pia amesema kikao cha juzi kiliamua mkutano mkuu wa klabu hiyo ufanyike Julai mwaka huu, na kwamba utatangazwa siku 30 kabla kwa mujibu wa katiba ya Simba, ambayo inaelekeza mkutano huo ufanyike mara moja kwa mwaka, hivyo hakuna sababu ya kuitisha mkutano wa dharura kwa sasa.
Mambo yamekuwa hayaendi vyema ndani ya kabu hiyo, hasa kutokana na mwenendo usioridhisha katika ligi kuu na mashindano ya Afrika, ambapo baadhi ya wanachama walitangaza kumng’oa Rage wakati akiwa India kwenye matibabu.
Hata hivyo, mapinduzi hayo hayakupata baraka za TFF, ambayo ilisema hivi karibuni kuwa mkutano uliodai kufanya mageuzi hayo ulikuwa batili.
No comments:
Post a Comment