Na Salum Vuai, Maelezo
BAADA ya kuwa katika mapumziko mafupi kupisha sherehe za tamasha la Pasaka, ligi kuu ya soka Zanzibar Grand Malt, leo inatarajiwa kurudi tena kwa mechi moja itakayochezwa uwanja wa Gombani, Pemba.
Pambano hilo linalotarajiwa kuwa kali na lenye ushindani kutokana na mazingira ya msimamo wa ligi hiyo sasa, litazikutanisha timu za Malindi na Jamhuri.
Ugumu wa mechi hiyo unatokana na hali mbaya inayowakabili masarahange wa Malindi, ambao watahitaji ushindi kwa uvumba na udi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kubaki katika ligi hiyo msimu ujao.
Malindi, iliyokwishacheza michezo 17 na kujikusanyia pointi 17 pia, iko katika nafasi ya kumi, na lazima ishinde mechi zake zote tano zilizobaki, kama inataka kuepuka kushuka daraja katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 12.
Aidha, katika upande mwengine, Jamhuri inahitaji kushinda kwani nayo haina uhakika wa kubaki salama kama itateleza katika michezo yake iliyobaki, kwa kuwa hadi sasa imeshindwa kuvuna pointi za kutosha kujihakikishia usalama wake.
Timu hiyo yenye maskani yake mjini Wete Pemba, hadi sasa imemudu kupata pointi 22 baada ya kushuka dimbani mara 16, na inajua vyema kuwa kama itafanya mzaha na kudondosha pointi, nayo huenda ikajikuta ikitoa nafasi kwa timu zilizoko chini ya msimamo kupanda, na yenyewe ikiteremka.
Baada ya mchezo huo wa leo, ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa pambano kati ya washika magendo wa KMKM wanaoongoza kwa pointi 37, na wajenga uchumi wa Duma wenye pointi 17, ambao pia wako katika vita vya kujinusuru kushuka daraja mwisho wa msimu.
No comments:
Post a Comment