Na Mwantanga Ame
SERIKALI inakusudia kufanya mabadiliko makubwa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, kwa kuondoa huduma kutoka katika mfumo wa kawaida na kwenda katika viwango vya kimataifa.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif Suleiman, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa dedha 2013/2014, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi.
Alisema serikali imeamua kufanya mabadiliko hayo kwa dhamira ya kuhakikisha uwanja huo unafuata sheria za kimataifa za utoaji wa huduma bora kama inavyofanywa na viwanja vyengine vya ndege duniani.
Alitaja baadhi ya mabadiliko hayo kuwa ni kuondoa mfumo wa sasa wa msongomano wa kupokea mizigo ya abiria kwani mfumo mpya utaweka mkanda maalum wa kusogeza mizigo hadi kwa muhusika.
Mabadiliko mengine ambayo aliyataja ni pamoja na kuimarisha eneo la kupokelea abiria na wadau wengine kwa kujengewa kipaa maalum kitakachotoka kwenye aneo ambalo wageni huwasili hadi sehemu ya maegesho ya magari ili kuwapunguzia usumbufu abiria na wapokea wageni kupiga jua na mvua.
Eneo jengine ambalo alilitaja ni ufanyaji wa mabadiliko katika mfumo wa mawasiliano kwa kuweka vipaza sauti katika sehemu za kuhudumia abiria ikiwa ni hatua ya kurahisisha mawasiliano ndani ya jengo.
Maeneo mengine yatahusu uwekaji wa mashine za X-rays kuhakikisha usalama wa mizigo na kuupandisha hadhi uwanja huo.
Alieleza mabadiliko mengine ni kuweka maeneo ya kituo cha biashara ndani ya kiwanja hicho ambapo yatasaidia nchi kuongeza kiwango cha ajira na mapato ya mamlaka hiyo na kujenga ukumbi mpya wa abiria wanaowasili wenye kiwango cha daraja la kwanza.
Alisema matumizi ya uwanja huo yameongezeka kutoka abiria 745,380 hadi kufikia abiria 774,669 mwaka 2012/2013 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 3.9.
Alisema kati ya abiria 708,863 walitumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Karume na 65,986 walikitumia uwanja wa ndege emba na waliounganisha safari zao walifikia 94,616.
Upande wa mizigo,alisema viwanja hivyo vilihudumia tani 1,159 ikilinganishwa na tani 900 kipindi kilichopita ikiwa ni sawa na asilimia 34 huku ndege zilizohudumiwa ni 55,499 ikilinganishwa na ndege 51,391, zilizohudumiwa mwaka 2011/2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.9.
Hata hivyo, alisema kuhusu ujenzi wa jengo jipya la kupokelea abiria tayari serikali imefikia makubalinao na Benki ya EXIM.
Alisema serikali ina dhamira ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara Unguja na Pemba zikiwemo za miradi.
Kuhusu ujenzi wa meli, alisema tayari serikali imeshatiliana saini na kampuni kutoka Korea kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya na inatarajiwa kufika nchini mwenzi Juni mwakani.
Kuhusu mradi wa mkonga wa taifa alisema tayari umekamilika na kampuni ya simu ya Zantel inaanza kutandaza huduma hizo katika maeneo mbali mbali ya Tanzania Bara, ikiwa pamoja na kuongeza vituo vya CDMA kutoka 79 hadi kufikia 116 ikiwa ni mpango wa kupeleka mawimbi maeneo ambayo bado yana matatizo.
Waziri huyo aliliomba baraza hilo, kumuidhinishia shilingi 20.092 bilioni ambapo kati ya fedha hizo shilingi 5.192 bilioni kwa kazi za kawaida na shilingi 14.90 bilioni kwa ajili ya kazi za maendeleo.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi, Panya Ali Abdalla, aliiomba wizara kufanikisha miradi inayoipanga ukiwemo wa ujenzi wa bandari ya Mpiga Duri kwa kuanza kuijenga kwa kutumia fedha za ndani wakati ikisubiri ufadhili.
Wakichangia wajumbe wa baraza hilo, walieleza hatua mbali mbali za ukuzaji wa huduma katika taasisi za wizara hiyo, ikiwemo eneo la uwanja wa ndege.
Mwakilishi wa Mkwajuni, Wadi Mussa Mtando, Hija Hassan Hija wa Kiwani, Mohammed Raza Dharamsi wa Uzini, Mwakilishi wa Chake Chake, Omar Ali Shehe, Salum Abdalla Hamad wa Mtambwe, Mwakilishi wa Magomeni, Salmin Awadh na Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma, wakikosoa baadhi ya huduma hizo ikiwa pamoja na kuhoji juu ya kuwepo malipo yanayotozwa kwa ajili ya kutumia eneo la wageni mashuhuri (VIP) na kusema hali hiyo inaweza kuwahamasisha watu wenye fedha kutumia eneo hilo kinyume na ilivyokusudiwa.
Aidha, wajumbe hao walikosoa juu ya suala la ujenzi wa barabara tatu za kisiwani Pemba zilizokwama kutokana na mkandarasi kutolipwa fedha zake.
Kutokana na kasoro hizo, baadhi ya wajumbe hao walikataa kuunga mkono bajeti hiyo na kutishia kuzuia baadhi ya vifungu.
Maeneo mengine yaliyotajwa kuwa na udhaifu ni Mamlaka ya Usafiri Bahari kwa kile walichodai imeshindwa kufanya kazi zake vizuri kutokana na baadhi ya meli za abiria zinazotoa huduma kutokuwa na vifaa muhimu.
Pia walidai imeshindwa kutoa baadhi ya vielelezo vya usajili meli ambapo kuna taarifa kwamba kuna meli za nje 406, ambazo zingeweza kutoa ajira 2030 ambapo kila mfanyakazi angelipwa mshahara wa dola za Marekani 2500 na kukusanya shilingi bilioni 8 kwa mwezi, ikiwa ni mapato yanayotokana na usajili wa meli hizo lakini taasisi hiyo ilishindwa kutoa taarifa hizo kwa kamati ya PAC ilipotaka ripoti hiyo.
Eneo jengine ambalo walilitaja ni viwango vya mishahara katika Mamlaka ya Uwanja wa Ndege kutokana na baadhi ya watumishi wa chini kulipwa shilingi 700,000 kwa mwezi, huku msimamizi mkuu akilipwa shilingi 600,000.
Nae Mwakilishi wa wanawake, Asha Bakari Makame, aliwataka wananchi kuwa na tabia ya kudai haki kwa mashirika ya ndege pale yanapowacheleweshea safari.

No comments:
Post a Comment