Na Fatuma Kitima, DSM
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewatahadharisha wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea uvunjifu wa amani na mifarakano katika jamii.
Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Profesa John Nkoma wakati wa kampeni ya kuhamasisha matumizi mazuri ya mawasiliano iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Alisema TCRA haitasita kuwachukulia hatua watu wenye tabia ya kutumia mitandao hiyo kuhamasisha kuvuruga amani, kuchonganisha watu, kusababisha ugomvi, kuwaumiza wengine kwa mambo yasiyo ya ukweli na kupotosha jamii.
Akizungumzia matumizi ya internet, alisema idadi ya Watanzania wanaotumia mtandao imeongezeka kutoka watu 300,000 hadi watumiaji milioni 7.6.
Alisema wengi wanatumia intaneti kujifunza, kujielimisha pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter, BBM, LinkedIn na Blog mbalimbali zinazotoa habari za kimaendeleo, burudani na michezo.
“Matumizi haya ya intaneti yamenufaisha Watanzania walio wengi kwani ni fursa murua ya kujifunza,” alisema.
“Kampeni hii, mamlaka inakusudia kuwasihi wananchi kuhakikisha wanatumia mawasiliano vizuri ili kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania,” alisema.
Kwa upande mwingine Profesa Nkoma alizindua wimbo wa video wenye ujumbe wa “Futa na delete meseji kabisa”, ambao umeandaliwa na wasanii Mrisho Mpoto na Banana Zorro wenye lengo la kuwataka wananchi kutumia mitandao ya kijamii vizuri.
Alisema mtu yeyote anaepokea ujumbe wowote wa kueneza chuki unaopelekea kuvuruga amani, atoe taarifa kwa vyombo husika.
ikiwa hivo , sasa uko wapi uhuru wa kusema kidemokrasia? katika demokrasia ya kweli inatakiwa uwe na upana wa kusikiliza kila kinachosemwa na kukizingatia kama ni kweli kinachosemwa au hapana , kuambiana ukweli ni lazima ikiwa ndugu profesa kama utakubali au hukubali sio muhimu , lakini kama ni mwadilifu inabidi ukubali kinachosemwa kama ni kizuri au kibaya na huko ndiko kupanuka kimawazo
ReplyDelete