Na Salum Vuai
BAADA ya kuridhishwa na
mafanikio yaliyopatikana katika Mradi wa Skuli inaoufadhili kupitia Jumuiya ya
Watu Wasioona Tanzania (TLB), taasisi ya 'My Right' ya nchini Sweden imeamua
kuongeza fedha katika awamu ya pili ya mradi huo.
Taasisi hiyo ambayo awali
iliitwa 'SRF' kabla kubadilishwa na kupewa jina jipya la 'My Right', imeongeza
fedha za mradi huo kufikia shilingi 200,000,022.
Fedha hizo hutolewa kwa
ajili ya kuwawezesha watoto wasioona na maalbino ambao ama wameacha skuli au
hawajapelekwa kabisa, kuandikishwa ili nao wapate haki ya elimu.
Akizungumza katika mkutano
wa maofisa wa Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB) kutoka wilayani
uliofanyika ofisini kwao Kikwajuni, mjumbe wa kamati inayosimamia mradi huo
Zanzibar Fatma Djaa Chesa, amesema
katika awamu ya kwanza mradi huo ulipewa shilingi 190,000,000.
Alifahamisha kuwa, takriban
watoto 100 wamenufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza ya miaka mitatu
iliyoanza mwaka 2011 na kumalizika mwaka 2013, ambao wamepelekwa skuli pamoja
na kupatiwa vifaa mbalimbali zikiwemo sare na viatu.
Akizungumzia utekelezaji wa
awamu hiyo ya kwanza, Fatma alisema kwa upande wa Unguja, walikuwa wakifanyia
kazi Wilaya ya Kusini, na kwa Pemba Wilaya ya Wete.
Alieleza kuwa, katika awamu
ya pili, ZANAB imeamua kutanua wigo na kuingia Wilaya ya Kati na Kaskazini A
Unguja, ambapo kwa Pemba Wilaya ya Wete itaendelea kuwa mlengwa mshiriki.
Hata hivyo, mjumbe huyo
ambaye anakaimu nafasi ya mratibu Adil Mohammed aliyeko Dodoma kwenye Bunge Maalum
la Katiba, alisema mradi huo unakabiliwa na changamoto kadhaa.
Aliitaja changamoto kubwa ni
kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa ngozi (maalbino), awali walikuwa
wakikataa kuwatoa watoto wao, kutokana na kushamiri kwa ukatili dhidi ya watu
wenye ulemavu kama huo huko Tanzania Bara.
Hata hivyo, aliishukuru
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za
kuwajengea mazingira mazuri watu wasioona na walemavu wengine, na kuitaka jamii
izidishe ushirikiano ili kutetea haki za kundi hilo.
Mapema, akizungumza na
washiriki wa mkutano huo, Naibu Katibu wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB)
Jonas Lubago, alisema awali wadhamini wao SRF walikuwa wakitoa ruzuku kwa ajili
ya kuendeshea shughuli za jumuiya zao Bara na Zanzibar, lakini kuanzia mwaka
2008 wameamua kutenga bajeti kwa ajili ya miradi maalum.
Lubago alieleza kuwa, kwa
upande wa Tanzania Bara, awamu ya kwanza iliweza kuwafikia watoto 81, ambao
sasa wanafurahia maendeleo mazuri katika skuli wengi wao wakiwa mabwenini.
Alieleza kuwa awamu ya pili
ya mradi huo unaoendeshwa kwa pamoja na Chama cha Maalbino, ZANAB na TLB, inaanza mwaka huu 2014 hadi 2017.

No comments:
Post a Comment